Nimatumaini yangu kila mmoja wenu atakuwa amejiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa mfumo wa kielektroniki wa BVR, anasubiri siku ya uchaguzi ifike ili aweze kumchagua kiongozi anayemtaka.
Nawapongeza sana kwa kufanikisha zoezi hilo licha ya kugubikwa na changamoto kibao ambazo awali zilikatisha tamaa, hongereni jamani kwa kupata vitambulisho hivyo muhimu, vitunzeni vizuri.
Baada ya kusema hayo sasa narejea kwenye jambo muhimu ambalo nimeona ni vyema kuzungumza nanyi kupitia safu hii mahususi kwa ajili ya kukumbushana, kuelimishana na kuwekana sawa pale inapobainika wapo wanaokosea sehemu flani.
Jambo lenyewe linahusu rangi za nguo za ndani kabisa zinazowavutia waume zetu lengo likiwa ni lilelile la kuboresha mashamsham ndani ya ndoa.Nasema hivyo, kwa sababu mwanamke anapovaa viwalo vya ndani vyenye rangi za kuvutia na mapigo ya kisasa, humpagawisha mumewe jambo hilo ndilo linalotakiwa.
Ni hivi shoga zangu, kwa uchunguzi nilioufanya kwa kufanya mahojiano na baadhi ya wenzetu na kwa kupitia kwa shemeji yenu, rangi nyeupe, pinki, krimu na zambarau zinapendwa sana na wanaume wengi.
Kwa mfano; mume wangu kila anaponiletea nguo hizo za ndani kabisa hajawahi kuninunulia nyeusi, nyekundu au njano, yeye asiponinunulia nyeupe itakuwa ya krimu au pinki.Siku moja baada ya kuniletea dazani ya nguo hizo nyeupe na pinki nikaamua kumuuliza sababu za kuzipenda rangi hizo akasema zinanipendeza nikivaa, nikacheka.
Shoga zangu, baada ya kubaini mume wangu anapenda rangi hizo nikaamua kufanya utafiti kwa baadhi ya shoga zetu ambao nao waliniambia waume zao wanapenda rangi hizo na zingine ambazo siyo za kung’aa sana.
Kutokana na uchunguzi huo, niwaase tu wenzetu ambao walikuwa hawaelewi siri hiyo, waanze kununua nguo za ndani kabisa za rangi hizo au kwa kuwauliza waume zao wanapenda rangi gani.
Pamoja na hilo, ni vyema kama wataanzisha utamadumu wa kuvaa nguo hizo za kisasa ambazo zitawasisimua waume zao jambo ambalo ndilo haswa linatakiwa katika ndoa. Bye.
Post a Comment