Mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amesema akichaguliwa na kuingia madarakani baada ya uchaguzi mkuu Oktoba 25, atahakikisha kuwa mikataba yote ya gesi na mafuta inapitiwa upya ili kuhakikisha kuwa kweli inawanufaisha Watanzania na siyo wawekezaji wa kigeni peke yao.
Lowassa
anayewakilisha pia muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) vya Chadema, NLD, NCCR-Mageuzi na Chama cha Wananchi
(CUF), aliyasema hayo jana mbele ya maelfu ya wananchi waliojitokeza
kusikiliza kampeni zake kwenye viwanja vya Mashujaa mjini hapa jana.
Alisema kwa kuanzia, ataunda tume ya kuchunguza upya mikataba ya gesi na mafuta.
Lowassa
aliongeza kuwa anafahamu kiu ya wananchi wa Mtwara kuhusiana na namna
wanavyokerwa juu ya kunufaika na rasilimali hizo ambazo ni chachu kubwa
ya maendeleo kwa wananchi na taifa kwa ujumla na pia ndoto yao ya kutaka
wanufaike na rasilimali hizo.
Alisema
wakazi wa Mtwara na Watanzania kwa ujumla, hawapaswi kuwa maskini
kutokana na kuwa na rasilimali nyingi kama gesi na mafuta na kwamba
akiingia madarakani atahakikisha maisha ya kila mwananchi yanapiga hatua
za kimaendeleo katika kila nyanja.
“Kama
mkinichagua, kila Mtanzania atanufaika... kama alikuwa anakula milo
miwili basi iongezeke na kuwa mitatu. Na kama anamiliki gari moja basi
awe na magari mawili. Nataka kuwa Rais wa nchi hii kwa sababu
nimechoshwa na umaskini wa taifa na wananchi wake,” alisema Lowassa.
Kadhalika,
Lowassa alirudia pia ahadi yake ya kuwaboreshea mazingira mazuri ya
kazi madereva wa bodaboda na wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kama
machinga na kina mamalishe.
Wote
hao aliwatambulisha kuwa ni marafiki zake na kwamba iwapo atachaguliwa
kuwa Rais, atahakikisha hawabughudhiwi katika kazi zao bali wanasaidiwa
ili nao wainuke kiuchumi.
Alisema
anafahamu ugumu na changamoto wanazokumbana nazo ambazo kwa kiasi
kikubwa zinachangiwa na serikali iliyopo madarakani ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM), akisisitiza kuwa wahifadhi vizuri shahada zao za
kupigia kura na kujitokeza kwa wingi kumchagua ili awatumikie.
Sumaye amvaa magufuli
Awali,
Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye alimtaka mgombea urais wa CCM,
Dk. John Magufuli, ahamie Ukawa na kuendelea na kampeni za kuing’oa CCM
madarakani kwani yaelekea ananogewa na kampeni zao na ndiyo maana
hutumia misemo yao, ikiwamo kubadili “Movement for Change’ (M4C) ya
Chadema kuwa ‘Magufuli for Change’.
Shughuli za simama
Katika
hatua nyingine, shughuli mbalimbali za biashara katika Soko Kuu la
Manispaa ya Mtwara Mikindani na maeneo mengine zilisimama kwa muda jana
baada ya wafanyabiashara kuamua kwenda kwenye viwanja vya Mashujaa
kusikiliza sera za Lowassa na Ukawa.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti kabla ya kufanyika kwa mkutano huo, baadhi ya
wafanyabiashara hao walisema kutokana na wanunuzi wengi kuwa katika
mkutano huo, wao hawana sababu ya kukaa katika biashara zao ila ni
kuungana na wananchi wengine kwenda kumsikiliza Lowassa.
Akizungumzia
hali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendegu, alisema kwa kuwa ni
maamuzi ya wafanyabiashara wenyewe kusitisha shughuli zao, hakukuwa na
sababu ya kuwazuia.
Dendegu
alikaririwa akisema katika kituo kimoja cha redio mjini hapa kuwa mtu
akisitisha biashara kwa hiari yake hakuna tatizo, bali kama kuna
shinikizo lolote kutoka miongoni mwao, sheria huchukuliwa dhidi ya
wahusika.
Post a Comment