
Mwanasiasa mkongwe na miongoni wa waasisi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kingunge Ngombale Mwiru jana alihutubia katika jukwaa la kampeni za Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na kusema chama tawala kimeishiwa pumzi.
Katika
mkutano wa kumnadi mgombea urais kwa tiketi ya Chadema na Ukawa, Edward
Lowassa katika viwanja vya Sinoni, mkoani Arusha, Kingunge alisema wale
wote wanaohoji uamuzi wake wa kuihama CCM atawajibu hivi karibuni.
Huku
akijinadi kuwa ni mwanabadiliko tangu kuasisiwa kwa CCM, mwanasiasa
huyo mkongwe nchini alisema sababu zinazoonyesha kuwa chama tawala
kimeishiwa pumzi ni kudorora kwa uchumi ambao kwa sasa unakuwa chini ya
asilimia saba.
“Hivi
karibuni hasa awamu hii ya sasa kuna dalili kuwa baada ya CCM kukaa
madarakani kwa nusu karne sasa imeanza kuishiwa pumzi. Rais Kikwete
amerithi uchumi ukiwa unakuwa kwa asilimia saba…sasa kwa mujibu wa
serikali yenyewe unakuwa kwa chini ya asilimia saba. Uchumi sasa
unadorora.”
Baada
ya kushuka jukwaani, mgombea urais Edward Lowassa alipanda jukwaani na
kuwataka wananchi wasichelewe kumpa kura ili akashughulikie matatizo
yanayowakabili ikiwemo afya, elimu, kuboresha mazingira ya biashara na
kukuza kipato cha wananchi.
Lowassa
alisema atahakikisha Tanzania inaendesha kilimo cha umwagiliaji na
kutoa uhuru kwa wakulima kuuza mazao yote kokote atapopenda tofauti na
hali ilivyo sasa.
Post a Comment