Wakati Lowassa akipata mapokezi hayo, Dk. Magufuli naye jana alitikisa ngome ya wapinzani, baada ya kupata mapokezi makubwa mkoani Kigoma.
Katika mji wa Chato, shughuli za kijamii zilisimama kwa saa kadhaa kutokana na sehemu kubwa ya wananchi kuhudhuria mkutano wa Lowassa.
Katika sehemu za maduka, baa, hoteli na migahawa biashara zilizorota kutokana na kukosa wateja kama ilivyo siku zote, hali iliyowafanya baadhi ya wafanyabiashara kulazimika kufunga biashara zao.
Wakati wa mkutano wa kampeni uliohutubia Lowassa katika uwanja wa stendi ya zamani mjini Chato, maelfu ya wakazi wa mji huo walikuwa wamehamasika na mara zote walikuwa wakishangilia.
Kutokana na hali hiyo, Lowassa alilazimika kukatisha hotuba yake mara kwa mara, ili kupisha kelele za washangiliaji.
Mapokezi hayo ambayo Lowassa, alisema hakuyatarajia nyumbani kwa mgombea urais wa CCM, alisema atafanya kila linalowezekana, arudi na timu yake mjini Chato kwa ajili ya kuhutubia mkutano mwingine wa kampeni.
“Nikitazama huu umma nashtuka, haya si mapenzi, bali ni mahaba, asanteni kwa mahaba, mnanifanya nideke nyumbani kwa Magufuli.
“Nimekuja kuwaomba kura ili niibadilishe nchi yetu kwa sababu nitakapoingia madarakani, nitaendesha nchi kwa spindi 150.
“Nilikopita kote mapokezi ni hivi hivi, hii ni neema ya mwenyezi Mungu, nataka nilete mabadiliko katika nchi yetu kwani elimu itakuwa bure kuanzia chekechea hadi chuo kikuu. “Nitaboresha maisha ya walimu na watumishi wote kwa kuwalipa vizuri kwani mambo haya yanawezekana kwa kuwa fedha hizo zipo.
“Ninataka kuleta mageuzi ya kweli si ya mchezo, kwa hiyo, naombeni kura zenu ili niweze kuongoza nchi hii,” alisema Lowassa.
Kuhusu suala la maji ambalo lilielezwa na mgombea ubunge wa Chato, Dk. Benedicto Rukanima (Chadema), alisema atakapoingia madarakani atawaletea maji hayo ikiwa ni pamoja na kukufua kiwanda cha pamba kilichokufa mjini Chato.
Pamoja na hayo, aliendelea kusema Serikali yake itakuwa rafiki kwa waendesha bodaboda, mama lishe, wamachinga na wachimbaji wadogo wadogo.
Sumaye
Naye waziri mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye, aliwataka wananchi hao wasimchague Dk. Magufuli kwa kuwa hana sifa za kuwa kiongozi.“Nasikia Magufuli aliwambia mkajisaidie haja kubwa barabarani ili mpate lami. Sasa kama alidiriki kusema hivyo akiwa mbunge na waziri, je akiwa rais hali itakuwaje?
“Msimpe kura kwa sababu hata yeye mwenyewe anakubali CCM imewakosea Watanzania ndiyo maana kwenye kampeni zake anasema kitanda kikiwa na kunguni msikichome moto,” alisema Lowassa.
Mwalimu afunguka
Wakati huo huo, Mwalimu wa Shule ya Sekondari Chato iliyoko Wilaya ya Chato, Lucas Michael, amemkaanga Dk. Magufuli, akisema kwamba hana sababu ya kuwaambia Watanzania wakajifunze Chato katika suala la Maendeleo kwa kuwa hakuna jambo la maana alililofanya.Mwalimu Michael ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Wilaya ya Chato, aliyasema hayo jana baada ya kupanda katika jukwaa la mkutano wa Lowassa.
Kwa mujibu wa Mwalimu Michael, Wilaya ya Chato ambako ndiko nyumbani kwa Dk. Magufuli, kuna matatizo mengi katika sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na walimu kuchanga fedha za kununua chaki.
“Tanganyika ilipata uhuru kutokana na jitihada za wazee wetu akina Nyerere na Kambona na kama walimu wasipopigania haki zao, haki hizo haziwezi kupatikana.
“Juzi nilimsikia Dk. Magufuli akisema kama Watanzania wanataka kujifunza maendeleo, waende Chato. Hivi Chato kuna nini? Chato ya Magufuli walimu hawaendelezwi kielimu, walimu wanachanga fedha za kununulia chaki na wanapostaafu hawasafirishwi kwenda kwao.
“Jamani kazi ya kwanza ya mwalimu ni kufundisha akiwa darasani na kazi nyingine ni kufundisha elimu ya watu wazima.
“Ndugu zangu walimu, ninachotaka kukisema hapa, mmeshakisema wenyewe, walimu msiwe waoga kwa sababu jukumu lenu ni kufundisha ukweli.
“Kwa hiyo, nawaomba walimu kote nchini mkafanye uamuzi sahihi, katika wakati sahihi na wakati ndiyo huu, pigeni kura vizuri, asanteni kwa kunisikiliza,” alisema Mwalimu Michael.
Mgufuli afunika
Naye mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli amepata mapokezi ya kihistoria mkoani Kigoma, baada ya maelfu ya wananchi kuhudhuria mkutano wake.Dk. Magufuli aliwasili mkoani Kigoma jana akitokea Tabora, alipopokewa na wananchi wengi waliokuwa wamejipanga pembezoni mwa barabara kuu ya Kigoma- Kasulu ambapo baadaye alifanya mkutano katika Uwanja wa Kawawa (Cine Atlas).
Akihutubia maelfu ya wananchi wa mji wa Kigoma na viunga vyake, Dk. Magufuli, alisema amejipanga kuwatumikia Watanzania kwa vitendo badala ya maneno.
Alisema ana shauku kubwa ya kuliongoza Taifa, huku akiahidi kuteua mawaziri ambao watakwenda na kasi yake katika kusukuma maendeleo ya nchi.
Alisema kama akishinda, anahitaji kuwa na mawaziri ambao watakuwa tayari kufanyakazi na hata kukemea rushwa katika majukumu yao.
Alisema anajua changamoto zinazowakabili wananchi wa mkoa huo, ikiwamo kuwa na reli ya kisasa ukosefu wa huduma za maji na umeme kwenye maeneo mengi, huku akiahidi kuyashughulikia kwa wakati akipewa ridhaa ya kuongoza nchi.
“Mmenipa mapokezi makubwa, nawaahidi sitawaangusha. Nitateua baraza la mawaziri ambalo litakwenda na kasi ya maendeleo mnayoyahitaji.
“Tena watasimamia, mimi mwenyewe pamoja na waziri mkuu makini na watakuwa tayari hata kung’atwa na mbu, kunguni wakati wote ili mradi wawatumikie Watanzania hata usiku wa manane.
“… ndiyo maana nasema hapa, mawaziri nitakaowateua kama mtanichagua kuwa rais wa awamu ya tano, wajiandae kufanyakazi kwelikweli, nataka kujenga Tanzania mpya. “Ndio maana hata picha zangu mimi Magufuli nimevaa shati na wengine wamevaa suti je wataweza kuja hapa na kusikiliza kero zenu, mimi kwangu ni kazi tu,” alisema Dk. Magufuli.
Dk. Kaborou akataliwa
Katika mkutano huo, upepo uligeuka baada ya Dk. Magufuli kuanza kumuombea kura mgombea ubunge wa Kigoma Mjini, Dk. Walid Aman Kaborou (CCM), ambapo wananchi walisikika wakisema. “Hatumtakiiii”.“Wewe Magufuli kura zako nyingi tutakupa, Kaborou hatumtakiiiii,” ilisikika sauti hiyo huku wakionyesha mikono ya kumkataa.
Hata hivyo, Dk. Magufuli aliwaomba wananchi hao kutofanya uamuzi wa jazba, badala yake wamchague mgombea huyo wa ubunge.
Kukataliwa kwa Dk. Kaborou kulianza kuonekana mapema, alipopewa nafasi ya kujieleza, kwani alijikuta akikumbana na kelele za kuzomewa.
“Pamoja na haya yanayoendelea hapa Kigoma Mjini, nataka kuwaambia jimbo hili si hifadhi ya kisiasa,”alisema Dk. Kaborou huku akizomewa.
Wakati huo huo habari kutoka Nzega zinasema, mgombea mwenza wa urais wa Chadema kupitia Ukawa, Juma Duni Haji, jana alilazimika kuwaomba wananchi wa Jimbo la Nzega Vijijini kumpigia kura mgombea ubunge wa CCM, Dk. Khamis Kigwangala, baada ya kumkataa mgombea ubunge wa CUF, Khamis Katuga.
Wananchi hao, wengi wakiwa wanachama wa Chadema, walisema wanamtaka Joseph Malongo wa Chadema.
Wakizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika katika Kata ya Ndala, Nzega Vijijini, wananchi hao walisema mgombea wa CUF hakubaliki.
Chokochoko zilianza baada ya Duni kumaliza kuhutubia na kumwita Katuga jukwaani ili amtambulishe, ambapo baadhi ya vijana waliokuwa na mabango upande mmoja walimshangilia na upande mwingine kumzomea.
Baada ya kuona hali hiyo, Duni alisema uamuzi wa Ukawa ni kumsimamisha mgombea wa CUF, kama hawataki wampigie Dk. Kigwangala. “Huyu ndiye aliyekubaliwa na Ukawa, kama hamtaki mpigieni Kigwangala,” alisema Duni huku akishangiliwa na vijana wachache waliokuwa na mabango.
Habari hii imeandaliwa na Maregesi Paul, Chato, Bakari Kimwanga, Kigoma na Elias Msuya, Nzega.
-Mtanzania
Post a Comment