Umoja wa Ulaya (EU), umesema Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu nchini, una ushindani mkali na siyo mwepesi kama chaguzi nne zilizopita chini ya mfumo wa vyama vingi.
Tangu
kuanza kampeni za Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu,
wagombea urais wanaoonekana kuchuana vikali ni wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Dk. John Magufuli na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa.
Akizungumza
jana jijini Dar es Salaam katika kongamano la amani lililoandaliwa na
Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (Moat) na Sekretarieti
ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Mkuu wa Ujumbe wa EU, Balozi
Filiberto Sebregondi, alisema chaguzi zilizopita jicho lao kubwa
lilikuwa Zanzibar kutokana na ushindani uliokuwapo.
“Zanzibar
hali ilikuwa ngumu kwa wakati ule, lakini siasa zimebadilika, uchaguzi
wa sasa ni wenye ushindani mkubwa, kampeni zinazoendelea ni zenye
ushindani, tuangalie joto la uchaguzi lisije kusababisha kutoweka kwa
amani,” alisema.
Alisema
hadi sasa EU inaridhishwa na mwenendo wa kampeni na kinachotakiwa ni
kwa wagombea kuendeleza kampeni za amani, kistaarabu na kuhakikisha kila
mmoja anawajibika katika nafasi yake.
Balozi
Sebregondi alisema hadi sasa waangalizi wao 34 wameshaingia nchini na
matarajio yao ni kuwa na waangalizi 134 katika wiki tano hadi sita kabla
na baada ya uchaguzi.
Alisema
chaguzi zilizopita waangalizi wa EU walielekezwa zaidi Zanzibar
kutokana na hali ya kisiasa iliyokuwapo, lakini kwa sasa watasambazwa
nchi nzima kutokana na hali ya kisiasa iliyopo.
“Kwa EU Uchaguzi Mkuu ni kipaumbele katika kuchangia ukuaji wa demokrasia,” alibainisha.
Kwa
mujibu wa Balozi Sebregondi, EU imeingiza kiasi cha Euro bilioni 1.2
kwa nchi za Afrika kwa ajili ya ulinzi na usalama, na kuhakikisha uwepo
wa amani.
Aidha,
alisema wakati wa uandikishaji wa wapigakura Zanzibar yalitokea
malalamiko mengi ambayo yangeandikwa kwa kina yangesaidia kupata
ufumbuzi.
Aliwataka
waandishi wa habari kutumia vizuri kalamu zao kwa kuripoti mambo yenye
kujenga amani pamoja na kuwakemea viongozi au wanasiasa wanaotaka
kusababisha machafuko.
Naye,
Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini, Alvaro Rodriguez,
alisema Jumuiya ya Kimataifa inafuatilia kwa karibu uchaguzi huo ili
kuisaidia Tanzania kuendelea kuvutia watalii, wawekezaji katika
maendeleo na kuongeza ajira, pamoja na kuendelea kuwa mdau wa maendeleo
na nchi ya kidemokrasia.
Alisema
migogoro ina gharama kubwa katika jamii kwa kuwa machafuko huaribu
miundombinu, kukimbiza wafanyabiashara, wawekezaji, watalii pamoja na
kupoteza kuaminiana ndani ya familia.
“Jamii
iliyotengwa kwa kukosa elimu, ajira na inayoishi katika maisha ya
chini, wanaweza kuandaliwa au kuwa waathirika wakubwa wa uvunjifu wa
amani pamoja na kuongeza ukatili kwa makundi ya wanawake na watoto."
Rodriguez
alisema UN imesaidia mafunzo kwa wawezeshaji wa haki za binadamu,
jinsia na nafasi ya jeshi la polisi wakati wa Uchaguzi Mkuu.
Alisema
maafisa wa polisi 103 walifundishwa kwa siku tano kuhusu masuala
mtambuka, haki za binadamu, jinsia, utatuzi wa migogoro, hatua za
uchaguzi, kukamata na matumizi ya vyombo vya moto.
“Kubwa
kinachoangaliwa kwa sasa ni nafasi ya Jeshi la Polisi wakati wa
Uchaguzi Mkuu na jinsi ya kufanya kazi na vyombo vya habari,” alisema.
Alisema
mafunzo hayo yatawafikia maafisa wa polisi 6,000 na kwamba matarajio ya
UN ni kufanya kazi kwa utaalamu, kutoa taarifa na kuzuia ukatili hasa
kwa makundi yaliyotengwa.
“Matarajio
yetu ni kuwa jitihada hizi zitachangia amani na uchaguzi huru kwa
wanawake, vijana na wenye ulemavu kushiriki katika uchaguzi kama
wagombea na wapigakura bila ukatili na unyanyasaji, na waandishi wa
habari kuripoti uchaguzi katika mazingira ya amani,” alisema.
Kwa
mujibu wa Rodriguez, wanashirikiana kwa karibu na Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (Nec) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) kuzisaidia katika
mchakato wa utangazaji matokeo ya uchaguzi, uwazi na kuzingatia muda
kama njia ya kuzuia migogoro katika uchaguzi huo.
Aliongeza
kuwa UN itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Serikali na Watanzania
kwa kuzingatia maono kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu.
Post a Comment