OFISI
ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, imeingia katika
kashfa nzito na kudaiwa kufanya ubadhirifu wa fedha za umma.
Hatua
hiyo inakuja wakati Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk.
John Magufuli inapambana na kudhibiti matumizi makubwa pamoja na vita
dhidi ya ufisadi.
Ofisi
hiyo ambayo inaongozwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG),
Profesa Juma Assad, imethibitika kufanya matumizi hayo pamoja na
matumizi mabaya ya madaraka.
Tangu
Profesa Assad alipoteuliwa kushika wadhifa huo Novemba 5, 2014 na
kuapishwa Desemba 2 mwaka huo na Rais mstaafu Jakaya Kikwete, ofisi hiyo
imebariki mambo kadhaa kinyume na maadili na majukumu yake.
Ukarabati wa Nyumba
Kwa
mujibu wa nyaraka zilizovuja, Aprili mwaka jana Ofisi ya CAG ilianza
mchakato wa kukarabati nyumba ya Serikali Plot namba 973 iliyopo
Mikocheni, Dar es Salaam inayotumiwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa
Serikali.
Kwa
mujibu wa taratibu, nyumba zote za Serikali zipo chini ya Wakala wa
Majengo ya Serikali (TBA) na taratibu zote za ukarabati hufanywa na
kusimamiwa na wakala huyo.
“Lakini
hapa kwetu hali ilikuwa tofauti kabisa, ofisi ya CAG iliamua kufanya
yenyewe ukarabati huku ikijua kabisa inakiuka utaratibu na ikatoa kazi
hiyo kwa kampuni bila hata kutangaza zabuni, hata kampuni husika haikuwa
na mkataba wowote na ofisi ya CAG.
“Cha
kushangaza zaidi kampuni hiyo ya M/SAfriq-Engineering and Construction
Co. Ltd si ya kigeni, ni ya Waswahili wenzetu, lakini ililipwa gharama
za kazi kwa dola za Marekani badala ya shilingi ya Tanzania.
“Na
si kwamba ililipwa kwa awamu kama ilivyo kawaida, bali wao walilipwa
jumla ya dola za Marekani 102,570 kwa mkupuo, tena hata kabla ya kuanza
kazi, ambapo pamoja na gharama zikiwamo kodi za Serikali, jumla ilifika
Sh milioni 281.8,” kilisema chanzo cha habari hii.
Kabla ya Profesa Assad kuingia katika nyumba hiyo, ilikuwa ikitumiwa na CAG aliyestaafu, Ludovick Utouh.
Ununuzi wa Samani za ndani
Pamoja
na hali hiyo ofisi hiyo ya CAG ilikiuka sheria na taratibu za Serikali
kutokana na kiongozi wa taasisi hiyo ya umma kulipwa posho ya Sh milioni
18 kwa ajili ya kununua samani za ndani ambazo hubadilishwa kila baada
ya miaka mitano.
Katika
kutekeleza stahiki yake hiyo, Profesa Assad alikwenda mwenyewe Umoja wa
Falme za Kiarabu (UAE) kwa kwa ajili ya kununua samani hizo za ndani
Desemba 27, mwaka juzi.
Inadaiwa
katika safari hiyo CAG alikiuka sheria na taratibu za Serikali kwa
kutumia zaidi ya Sh milioni 18, ambazo zinaruhusiwa kwa “KUNDI A” la
viongozi kwa mujibu wa waraka wa Idara Kuu ya Utumishi (Ofisi ya Rais)
namba 1 wa mwaka 2014.
Baada
ya kununua samani hizo, ofisi yake ililipa fedha za ziada kiasi cha Sh
milioni saba kwa ajili ya kuzisafirisha, pamoja na dola za Marekani
4,265 (sawa na shilingi milioni 9) kwa ajili ya kodi, visa na gharama
nyingine za usafiri.
Uununuzi wa Shangingi
Mei
13, 2015 ofisi hiyo ya CAG ilimwandikia barua Mtendaji Mkuu wa Wakala
wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA) barua yenye kumbukumbu namba FA.242/305/01 yenye kichwa cha habari; “UNUNUZI WA GARI MOJA KWA AJILI YA MATUMIZI YA CAG TOYOTA LAND CRUISER GX-V8 200 HIGH.”
Baada
ya Mtendaji Mkuu wa GPSA, J. Mwambega kupokea barua ya ombi hilo,
alimjibu kwa barua ya Mei 15, mwaka jana, yenye kumbukumbu Na. CAD.124/318/01/64.
Sehemu ya barua hiyo ambayo nakala ilipelekwa kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha inasomeka; “Napenda
kukujulisha kwamba ombi lako la ununuzi wa dharura halikubaliki kwa
sasa kwa sababu upo utaratibu ulioandaliwa na Serikali kwa ajili ya
ununuzi wa magari ya viongozi.
“Kwa
kuzingatia hilo, nakushauri ulipie gharama za ununuzi wa gari hilo US $
84,480.05 kupitia akaunti ya GPSA – UNUNUZI WA MAGARI KWA PAMOJA yenye
Na. 0250095100500 ‘US$ Account’ iliyopo benki ya CRDB Bank (Plc) Tawi la
Vijana, Dar es Salaam.”
Pamoja
na maelekezo hayo, ofisi hiyo ya CAG ilikiuka maelekezo ya Mtendaji
Mkuu wa GPSA na kununua gari hilo kwa dharura, ambapo malipo yalifanyika
Mei, 15, 2015.
Safari ya Seychelles, China
Septemba
5, mwaka jana maofisa kadhaa akiwamo Profesa Assad walisafiri kikazi
kwenda nchini Seychelles, ambapo Septemba 11, waliondoka nchini humo na
kwenda Dubai, Septemba 12 waliondoka Dubai kwenda Nanjing (China),
Septemba 19, waliondoka Shanghai kwenda Beijing na Septemba 22,
waliondoka Beijing kurejea Dar es Salaam.
Uchunguzi
umebaini kuwa ukiacha safari ya Seychelles ambako kulikuwa na mkutano
wa wakaguzi wa hesabu, safari ya China haikuwa na uhusiano na majukumu
ya kiofisi, ambapo tiketi za ndege ziligharimu Sh milioni 26.4.
Mbali
ya CAG, ofisa mwingine kutoka ofisi yake, Edwin Rweyemamu, naye
alisafiri kwa mzunguko kama huo, ambapo tiketi yake iligharimu Sh mil
21.7.
Ofisa
wa tatu ambaye hakwenda Seychelles, lakini aliambatana na CAG
kwingineko ni Elibariki Lyatuu, ambaye tiketi yake iligharimu Sh milioni
21.4.
Wote
walisafiri kwa kutumia daraja la “Business Class” ambapo jumla ya
gharama za tiketi zote tatu ilikuwa Sh mil 69.6, gharama ambazo
zinatajwa kuwa kubwa kulinganisha na gharama halisi za safari kwenda
nchi hizo, gharama ambazo hubadilika kutegemea na msimu wa safari.
Uchunguzi
ulibaini fedha hizo zilikopwa kutoka fungu la fedha za Umoja wa Mataifa
(UN) zinazotumika katika shughuli mbalimbali ya ukaguzi wa hesabu,
ambapo ofisi ya uhasibu ilisema katika dokezo.
Dokezo
hilo linasomeka; “Lipa Sh 69,659,200 kwa ajili ya tiketi za safari ya
CAG na ujumbe wake nchini Seychelles na China. Fedha hii ilipwe toka UN,
lakini tukumbuke kuirudisha mara tutakapopokea mgawo wa fedha ujao.”
Kauli ya CAG
Apotafutwa Profesa Assad Alhamisi iliyopita ofisini kwake, alikataa kujadili au kuzitolea ufafanuzi tuhuma dhidi yake.
“Kwanza
unajua ni makosa kuwa na nyaraka za ofisi ya Serikali, sasa kama
ukiandika basi na sisi tutachukua hatua. Pia hayo yote uliyosema mimi
sihusiki, watafute watendaji wakupe majibu,” alisema Profesa Assad.
Pamoja na kutoa majibu hayo, alisema atahakikisha anampata mfanyakazi anayetoa siri za ofisi na kumfukuza kazi mara moja.
Baada
ya mwandishi kuagana na CAG na kuondoka, akiwa nje ya ofisi hizo, ofisa
mmoja ambaye alihudhuria mahojiano hayo, alimwita na kumwomba nakala ya
nyaraka husika, ambapo alipewa, lakini hakuna majibu au maelezo yoyote
ambayo yalitoka baada ya hapo.
Chanzo: Mtanzania
Post a Comment