RAIS Jakaya Kikwete jana aliagwa kifalme katika ziara yake ya kikazi nchini Uholanzi, huku akielezea kwa kiasi kikubwa mafanikio ya utawala wake katika miaka kumi aliyokaa madarakani.
Kikwete aliyewasili juzi usiku mjini hapa akitokea katika ziara yake ya nchi za Finland, Denmark na Sweden, alipokelewa na kupewa heshima zote za kifalme, ikiwa ni pamoja na kupewa makazi katika kasri la Mfalme, akiwa kiongozi wa tatu wa Afrika kupewa hadhi hiyo nchini hapa.
Wengine waliowahi kupewa hadhi hiyo ni Rais wa Kwanza mzalendo wa Afrika Kusini, Hayati Nelson Mandela na Askofu Mkuu mstaafu wa mji wa Cape Town, Afrika Kusini na mshindi wa tuzo la Nobel Desmond, Desmond Tutu.
Rais Kikwete baada ya kukutana na Balozi wa Tanzania nchini hapa, Wilson Masilingi na maofisa wake, alianza kazi kwa vikao na wawekezaji, ikiwemo kampuni ya Shell, alikutana pia na kuzungumza na Mfalme Willem Alexander na baadaye alikutana na Rais wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) katika makao makuu ya mahakama hiyo, Silvia Alejandra Fernandes de Gurmendi.
Jioni alikutana na mabalozi wa Afrika, wanaowakilisha nchi zao nchini Uholanzi, ambapo alitumia fursa hiyo kuwaaga, akiwataka wampe ushirikiano rais ajaye, lakini pia alielezea mafanikio makubwa aliyoyapata katika utawala wake.
Alisema ingawa anaondoka madarakani baada ya utawala wake wa miaka kumi, anaamini Tanzania itapata kiongozi mzuri licha ya mchuano mkubwa unaoendelea, akisema alikuwa na taarifa kuwapo kwa makada 34 wa CCM wanaowania kutaka kumrithi.
“Ninamaliza muda wangu, hivyo napita kuaga marafiki na nchi wahisani. Tuna historia ndefu na Uholanzi, tangu enzi za Nyerere (Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere). Babu wa huyu Mfalme (Willem) alikuwa na shamba Tanzania, lakini pia baba yake amesoma Tanzania. Hawa ni ndugu zetu,” alisema na kuishukuru Serikali ya kifalme ya Uholanzi kwa kumpa mwaliko rasmi wa kikazi.
Hata hivyo, Rais Kikwete alipokuwa akizungumzia kasi ya kuondoa umasikini, alisema bado juhudi za kuondoa umasikini zinahitajika na zitafanikiwa kwa kuelekeza nguvu kwenye kilimo, ambacho ndicho kinachoajiri na kutegemewa na Watanzania wengi zaidi hasa wanaoishi vijijini.
Rais Kikwete pia amefanya mazungumzo na Spika wa Bunge la Sweden, Urban Ahlin, pamoja na viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa nchini humo na kushukuru kwa misaada ya maendeleo kwa takribani miaka 50Nsasa.
Mabalozi hao wa Afrika wamempongeza Rais Kikwete kwa kufanya ziara ya shukrani na kuwaaga nchi rafiki na wahisani, kwani ni mara chache kwa viongozi wengi wa Kiafrika kuaga na kuondoka madarakani.
Kwa upande wa elimu, alisema wakati akiingia madarakani mwaka 2005, alikuta Tanzania, yenye watu wengi zaidi katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), iko nyuma ikilinganishwa na Kenya na Uganda, kwa idadi ya wanafunzi waliokuwa wakisoma shule za sekondari na vyuo.
Kwa upande wa elimu ya juu, Rais Kikwete alisema vyuo vikuu vimeongezeka kutoka 26 mwaka 2005 hadi kufikia 52 na idadi ya wanafunzi walio katika vyuo vikuu ilitoka 40,719 hadi kufikia 200,956.
Hata bajeti ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu imeongezeka kutoka Sh bilioni 56.1 hadi Sh bilioni 345 mwaka 2014. Rais Kikwete anatarajiwa kurejea nyumbani leo.
Post a Comment