VIJANA
wa Chama cha Wananchi kupitia jumuiya yao (JUVI-CUF) wameweka msimamo
kuwa ‘iwe iwavyo’ watafanya maandamano kesho visiwani humo kwa kuwa ni
haki yao kufanya hivyo licha ya Jeshi la Polisi kupinga.
Maandamano
hayo yameelezwa kuwa ni sehemu kumbukumbu ya Wazanzibari waliouawa
mwaka 2000 kutokana na vurugu za kisiasa zilizotokea chini ya Serikali
ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Maandamano
hayo yametangazwa ikiwa ni siku chache baada ya Mwenyekiti wa Tume ya
Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kutangaza tarehe 20 Machi
mwaka huu kuwa siku ya kurudia uchaguzi visiwani humo.
Jecha
alifuta matokeo ya uchaguzi mkuu visiwani humo uliofanyika tarehe 25
Oktoba mwaka jana kwa madai ya kuwepo kwa kasoro mbalimbali jambo ambalo
lilipingwa na CUF, taasisi za kiraia na baadhi ya makada wa CCM.
JUVI-CUF
wamepanga kufanya maandamano makubwa visiwani humo kwa lengo la kupinga
dhuluma hiyo licha ya Jeshi la Polisi kuyagomea.
Wameeleza
kuwa maandamano hayo watayafanya ili kuieleza dunia kwamba, Zanzibar
haki inaminywa na kwamba, maandamano hayo yatakakuwa ujumbe mahsusi kwa
wapenda demokrasia duniani.
Vijana
hao wamesema kuwa, hawawezi kuona haki yao inapokwa na serikali kwa
maslahi ya CCM na kwamba, maandamano hayo yatafanyika visiwani humo kama
ilivyopangwa.
Mkurugenzi
wa Habari na Mawasiliano wa JUVI-CUF, Abeid Ali amesema kuwa, wananchi
wa visiwa hivyo hawatokoma kudai haki yao mpaka pale itakaposimama.
Mkurugenzi
huyo ameeleza kwamba, wana imani kuwa si risasi wala mizinga ambayo
inaweza kusimamisha haki visiwani humo na kwamba, watapigania haki hata
kama wengine watauawa.
Kiongozi
huyo amekumbushia mauaji yaliyofanywa na Serikali ya Rais Mstaafu,
Benjamin Mkapa baada ya Uchaguzi Mkuu 2000 na kwamba, wananchi
hawajaingia woga wala kurudi nyuma kudai haki yao.
“Sisi
ni raia wakizanzibari, tuna uhuru wa kuandamana kwani CCM waliachiwa
kuandamana na ulinzi wakapewa, na sisi tuna haki ya kufanya maandamano,” amesema Ali.
Amesema kuwa, maandamano hayo yatafanyika kuanzia Mtendeni kwenda Mnazimmoja na kumalizikia kwenye viwanja vya Maisara.
Post a Comment