
KATIKA
kukabiliana na madereva wa pikipiki wanaopakia abiria zaidi ya mmoja
maarufu mshikaki, Jeshi la Polisi mkoani Pwani litatumia mbinu mpya ya
kuwapiga picha madereva hao na kuwakamata baadaye wakiwa kwenye vituo
vyao.
Jeshi
hilo litatumia mbinu hiyo ili kuepusha ukamataji kwa kuwakimbiza wale
wanaofanya hivyo kwa lengo la kuepuka kusababisha ajali wakati wa
kuwakamata madereva hao wanaobeba mshikaki.
Akizungumza
na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha, Kamanda wa Polisi
mkoani Pwani, Bonaventura Mushongi alisema kuwa mbinu hiyo itasaidia
kuwabaini na kuwapiga faini kwa mujibu wa sheria.
“Tumeona
tufanye hivyo kwani ukamataji wa zamani wa kufukuzana siyo mzuri,
unaweza ukasababisha ajali kwa wanaotumia pikipiki hiyo na hata kugonga
watu au mali katika kukwepa mkono wa sheria lakini kwa kuwapiga picha
tutawatafuta na kuwakamata wakiwa hawana abiria,” alisema.
Alisema
mbali ya kukamata madereva bodaboda wanaobeba mshikaki ambayo ni
kinyume cha sheria, pia watawakamata kwa makosa mengine kama vile
leseni, kutokuwa na kofia mbili ngumu na kutozingatia sheria za
uendeshaji na usalama barabarani.
“Pia
tunawaomba waendesha bodaboda watupe ushirikiano katika kubaini
wahalifu ambao wamekuwa wakitumia usafiri huo kufanikisha wizi hivyo
wanapaswa kutupa taarifa za watu wanaopanga kwenda kufanya uhalifu
kutumia vyombo hivyo,” alisema Mushongi.
Aidha
alisema kuwa endapo madereva hao wa bodaboda watatoa ushirikiano kwa
polisi itasaidia sana kukabiliana na uhalifu ambao umekuwa ukijitokeza
mara kwa mara.
“Pia
kuna taarifa kuwa baadhi ya waendesha bodaboda nao wanajihusisha na
uhalifu, tunawataka waache vitendo hivyo kwani wao ni watoa huduma na
endapo watabainika kufanya hivyo watakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo
vya sheria,” alisema Mushongi.
Alibainisha
kuwa jeshi lake litashirikiana na viongozi wa bodaboda katika
kuhakikisha kuwa wanafuata sheria na kupambana na uhalifu na siyo wao
kuwa chanzo cha uhalifu na kuvunja sheria.
Post a Comment