WIKI iliyopita tulijadiliana kuhusu wapenzi wenye tabia ya kuwaacha wenzi wao na baadaye kulazimisha kuwarudia kwa nguvu na vitisho baada ya kugundua ndiyo wapenzi sahihi wa maisha yao.
Leo tunazungumzia mada inayosema, je, mapenzi ni vita? Ungana nami kujua mengi zaidi kupitia XXLove.
Nianze kwa kuwashukuru wasomaji wangu kwa kunitumia ujumbe mfupi wa ‘SMS’ na kunipigia simu, asanteni.
Kwenye mada ya leo ni dhahiri kuwa majibu ya haraka ya walio wengi ni lazima yatakuwa ndiyo au hapana na majibu hayo yako katika pande mbili kwa maana ya waliofurahia na walioumizwa kwa sababu ya mapenzi.
Hivi kweli mapenzi ni vita? Kama ni vita ya nani na nani? Na nini chanzo cha vita hiyo? Kama ni vita kwa nini watu bado wanajiingiza kwenye vita hiyo?
Kama hapana, mbona wengine wanauawa kisa mapenzi, kama unakataa mbona mama, baba, ndugu, rafiki au baadhi yetu hatuelewani na familia zetu kwa sababu ya mapenzi au uhusiano wako na fulani?
Wengine wanafungwa kwa sababu ya mapenzi na hata wengine wanajeruhiwa au kujeruhiana, kisa mapenzi. Ndugu na marafiki hawatembeleani kwa sababu ya ugomvi wa mapenzi.
Ukweli uko hivi; kuna wakati penzi huwa tamu sana kuzidi asali na wakati mwingine huwa chungu zaidi ya shubiri. Namaanisha hivi; kuna watu wengine wanafurahia uhusiano walio nao na wapenzi wao huku wengine wakionekana kujuta kwa nini hawakujuana mapema ili kufaidi raha hizo mapema.
Wakati huohuo, kuna wapenzi wengine wanajuta kuingia katika uhusiano na mpenzi huyo, yawezekana kwa kulazimishwa au yeye mwenyewe kupenda lakini leo anajuta. Anatamani aachike ili ajinasue lakini inakuwa ngumu.
Kwa wanaofurahia hawataona kuwa mapenzi ni vita lakini kwa walioumizwa, wataona ni vita kwa sababu yawezekana waliumizwa au wanaumizwa kila kukicha, wengi wanashindwa kuendelea na masomo yao, kisa kikiwa ni mapenzi, binti au kijana kashindwa au kafukuzwa nyumbani kwao chanzo kikiwa ni uhusiano na mtu fulani. Wengine wanafeli mitihani yao kwa sababu mpenzi wake kamchanganya.
Mara nyingi mpenzi msomaji, umekuwa ukisikia juu ya watu wanaolalamikia mapenzi kama chanzo cha kuharibika kwa maisha yao na mipango yao na kuyaona mapenzi kama vita. Ni vyema ukajua kuzungumza na moyo wako ili kufanya lililo sahihi kwenye uhusiano wako.
Tukutane wiki ijayo kwa somo lingine murua.
Post a Comment