MBUNGE wa Ilala, Mussa Zungu (CCM), amesema kutokana na tatizo la ukosefu wa ajira linalowakabili vijana wengi nchini, ni lazima rais ajaye awe na ajenda maalumu ya kukabiliana nalo.
Zungu alisema hayo juzi jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla ya kuwaaga wanafunzi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) waliomaliza ngazi ya Cheti, Shahada na Astashahada ambao ni makada wa chama hicho.
“Ukosefu wa ajira ni tatizo ambalo lipo kila mahali hadi Ulaya na si Tanzania pekee, lakini linaweza kutatulika iwapo tutakuwa na ajenda maalumu ya kusaidia vijana wetu ili waweze kujiajiri na kuachana na mawazo ya kuajiriwa,” alisema.
Alisema iwapo atafanikiwa kushinda nafasi ya ubunge kwenye Uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka huu na kuendelea kuongoza jimbo hilo, ataendelea kusisitiza juu ya jambo hilo.
“Katika Bunge hili la hivi sasa niliwahi kupendekeza kwamba lazima kuwepo na bajeti maalumu ambayo itawekwa kwenye mfuko wa kusaidia vijana, nilipendekeza kiasi cha Sh bilioni 200 ili waweze kukopa na kujiajiri.
“Nina uhakika kwamba nitashinda na kurudi bungeni tena na nitakwenda kuendelea kutetea hoja yangu hii, kwa hiyo natoa rai kwa wapiga kura katika jimbo langu kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura pindi Tume ya Uchaguzi (NEC) itakapofika hapa Dar es Salaam ili waweze kunipigia kura wakati utakapofika,” alisema.
Post a Comment