MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu leo, imewahukumu kifungo cha miaka mitatu jela aliyekuwa Waziri wa Fedha na Uchumi, Bazil Mramba na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona baada ya kuwatia hatiani kwa makosa mawili.
Akizungumzia hukumu hiyo, Wakili wa washtakiwa hao, Peter Swai, amesema kwamba hukumu hiyo imetolewa na jopo la majaji watatu ambao ni Jaji Samu Rumanyika, Jaji John Utamwa, pamoja na Hakimu Saul Kinemela, ambapo mtuhumiwa wa tatu wa kesi hiyo ambaye ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja, amekutwa hana hatia huku mawakili wa washtakiwa wakiazimia kukata rufaa.
“Hatujaridhika na hukumu ila shauri limesikilizwa na Mahakimu wa tatu. Na kwa mujibu wa sheria tukikata rufaa aidha watakubali wote watatu au mmoja wao atakataa, kwahiyo iwapo mmoja wao atakataa na wawili wakikubaliana hiyo ndiyo hukumu ya Mahakama, na hicho ndicho Mahakama ilichofanya leo, hili ni jambo la kisheria kama tunaamini kwamba uamuzi uliotolewa hauendani na sheria tutakata rufaa kwenye Mahakama ya juu na itatafsiri sheria upya na sisi tutapata majibu”amesema Swai.
Kwa mujibu wa sheria ya makosa ya jinai, kosa la matumizi mabaya ya madaraka adhabu zake ni kulipa faini ya Sh. milioni 2 au kifungo cha kati ya mwaka mmoja au miaka mitatu jela baada ya mshtakiwa kupatikana na hatia.
Katika mashtaka hayo ilidaiwa kuwa washtakiwa wakiwa watumishi wa serikali, Oktoba 10, mwaka 2003 walikaidi ushauri wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wa kuwataka wasitoe msamaha kwa Kampuni ya Alex Sterwart (Assayers) Government Business Corporation.
Novemba 25, mwaka 2008, washtakiwa hao, walifikishwa katika mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Hezron Mwankenja, na kusomewa mashitaka 13, likiwamo la matumizi mabaya ya madaraka. Kesi hiyo ilipangiwa jopo hilo na kuanza kuisikilizwa mapema mwaka 2009.
Kumbukumbu zinaonyesha kwamba katika mashitaka yaliyokuwa yanawakabili washtakiwa ni pamoja na kudaiwa kati ya Agosti mwaka 2002 na Juni 14 mwaka 2004 Jijini Dar es Salaam, washitakiwa wakiwa watumishi wa umma kama Mawaziri walitumia vibaya madaraka. Mramba na Yona wanadaiwa kuwa kati ya Juni 2003 na Mei 2005, wakiwa na nyadhifa hizo za uwaziri kwa makusudi na kutowajibika waliruhusu mkataba wa kuzuia kulipa kodi ili kuipendelea kampuni hiyo na kuisababishia serikali hasara ya Sh. 11,752,350,148.00.
Washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh. Bilioni 11.7 kutokana na kutoa msamaha wa kodi kwa Kampuni ya kukagua madini ya dhahabu ya Alex Stewart (ASSAYERS) ya Uingereza iliyoingia mkataba wa kudhibiti madini ambapo kwa kupitia kampuni tanzu ya Alex Stewart (ASSAYERS) Government Business Corporation waliingia mkataba na kampuni tanzu kukagua uzalishaji wa madini ya dhahabu, kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya Umma.
Post a Comment