Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imelaani wanasiasa
wanaoingilia utendaji katika Sekta ya Afya kwa kutoa adhabu kwa
madaktari na wauguzi, bila kushirikisha vyombo vyao.
Wakizungumza
katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jana, wajumbe hao waliitaka
Serikali kuepuka unyanyasaji dhidi ya madaktari na wauguzi ili kurudisha
amani iliyokuwapo katika sekta hiyo.
Kamati hiyo ilimbana kwa
maswali Naibu Waziri wa Afya, Dk Hamis Kigwangalla ambaye alijitetea
hajahusika kusimamisha madaktari na wauguzi tangu Serikali ya Awamu ya
Tano ilipoingia madarakani.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Peter
Serukamba alipongeza hatua ya Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kuingilia
kati suala hilo kwa kutoa tamko la Serikali.
Alisema analaani
pia Watanzania wote ambao wanachukua sheria mkononi na kuwaadhibu
madaktari, akisema tabia hiyo haifai kuvumiliwa.
“Madaktari na
wauguzi wana chombo chao. Kama wamekosea tuwapeleke kwenye vyombo vyao
watapewa onyo au kuchukuliwa hatua za kinidhamu, jamani tuache siasa
kwenye Sekta ya Afya,” alisema Serukamba.
Alisema watoa huduma
ya afya wana umuhimu mkubwa katika jamii, lakini siku za hivi karibuni
wameonekana kunyooshewa vidole kwa kila jambo wanalolifanya na kuifanya
sekta hiyo yenye watumishi wachache kukosa molari.
Akijibu hoja
hiyo, Dk Kigwangalla alisema katika kulinda hadhi ya madaktari suala la
wananchi kujichukulia sheria mikononi limeikera sana Wizara ya Afya.
Alisema
wananchi wamepewa fursa ya kutoa maoni yao katika kila hospitali na
kituo cha huduma za afya, hivyo wanapaswa kutoa malalamiko yao na kama
watahitaji usiri wafunge katika bahasha maalumu.
“Nitumie nafasi
hii kuwataka wananchi wafuate taratibu kadri zilivyowekwa kwa mujibu wa
sheria kufikisha malalamiko yao,” alisema Dk Kigwangalla.
Kamati hiyo ilihoji sababu za jengo la Taasisi ya Mifupa (MOI) kuanza kutumika kabla ya ujenzi kukamilika.
Dk
Kigwangalla, baada ya kubanwa na kamati hiyo iliyosema kuna mgogoro
kati ya mkandarasi anayejenga na taasisi hiyo, aliuagiza uongozi wa MOI
kumpa taarifa sahihi kuhusu mkandarasi huyo.
Post a Comment