Marehemu Chacha Wangwe |
MTOTO wa marehemu, Chacha Wangwe, Zakayo Wangwe, ambaye alitangaza nia ya kugombea ubunge Jimbo la Tarime hivi karibuni, amebadili mawazo na kutangaza kugombea udiwani Kata ya Turwa.
Uamuzi huo aliuchukua jana na kuwaeleza waandishi wa habari kwamba, amejitathmini na kuona agombee udiwani badala ya ubunge.
“Nimepokea simu na meseji nyingi kutoka kwa watu wangu wa karibu, wengine wamenishauri lakini mwisho wa siku naweka wazi kwamba nia yangu ya kugombea ubunge nimeona niachane nayo ila nigombee udiwani.
''Yapo mambo mengi yaliyotokea baada ya kutangaza nia yangu ambayo kimsingi nayachukulia kama mapambano ya kisiasa licha ya kuwa na athari hasi kwangu, lakini maamuzi yangu sasa ni udiwani,''alisema Zakayo.
Zakayo alisema uamuzi huo umetokana na ushauri mwingi kutoka kwa familia, ndugu, marafiki, wanachama wenzake wa Chadema na watu mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tarime wa kumtaka kugombea udiwani badala ya ubunge kama ilivyokuwa kwa marehemu baba yake, Wangwe.
Alisema wakati wa uhai wa baba yake, aliwahi kushauriwa kugombea udiwani badala ya ubunge na kukubali na alifanikiwa kupata na baadaye aligombea ubunge na kushinda, hivyo anafuata nyayo za baba yake.
“Ningeweza kusimamia msimamo wangu hasa baada ya majimbo kugawanywa, lakini natambua fika thamani ya busara, nasaha na maono ya watu wanaonizunguka, natambua pia kiongozi bora ni yule aliye msikivu na aliye tayari kukosolewa na wananchi wenzake,”alisema.
Post a Comment