Kutoka kushoto DC Nawanda, Mwenyekiti wa Kijiji, DED Vavunge na KATIBU wa Afya aliyemwakilisha Mganga Mkuu wa Wilaya.
Wananchi wakimsikiliza DED wa Lindi Vijijini Bibi Olliver Vavunge (hayupo pichani) ktk kikao cha kutatua hali ya sintofahamu iliyodumu kwa wiki sasa ya wananchi kurusha mawe kituoni hapo kwa watumishi wake hali iliyozua hofu na kufanya kazi kwa woga.
Na Mwandishi Wetu, Nyangamara - Lindi
Mkuu wa Wilaya ya Lindi Mh. Yahaya Nawanda amelazimika kwenda kuongea na wananchi wa Vijiji vya Nyangamara B na Nyangamara A vilivyopo kwa pamoja kwa lengo la kujua matatizo yao kuhusiana na chuki iliyopo kati yao na watumishi wa Afya na waalimu waliopo katika Kituo cha Afya Nyangamara na waalimu wa shule ya Msingi ya Nyangamara.Mh. Nawanda akiongozana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Lindi pamoja na Kaimu Mganga Mkuu Wilaya Ndugu Langula Madirisha ambaye pia ni Katibu wa Afya wa Halmashauri hiyo walihoji matatizo yaliyopo kijijini hapo bila mafanikio yoyote hali iliyowashangaza wao na wahudhuriaji wengine.
Tatizo lililopo ni kwamba kuna Mawe yanarushwa kila siku ifikapo kuanzia saa 12 jioni na kuaendelea usiku mzima huku
walengwa yakiwa ni majengo pamoja na watumishi wenyewe katika kituo hicho, kiasi cha wengine kujeruhiwa. Hali ya kushangaza zaidi inapotokea hali hiyo ya urusaji mawe hayo hakuna mtu anayeonekana kuyarusha, Hivyo kupelekea kuhusishwa na Imani za kishirikina.
Taarifa zaidi zinadai kuwa Mwalimu mmoja wa shule ya Msingi naye alitolewa ngeu wakati wa "mashambulizi" hayo yaliyolenga shule yake.
Wananchi wa vijiji hivyo walipohojiwa na uongozi uliotembelea hapo walidai kuwa hata wao inawashangaza kuona hali hiyo inatokea kwa kuwa mshambuliaji haonekani hivyo inawezekana Watumishi wenyewe kwa wenyewe wanarushiana mawe hayo. Walipohojiwa iweje sasa Kituo cha Afya na Shule ziko mbali mbali na huyo Mwalimu amejeruhiwaje? hakuna aliyetoa jibu wote walinyamaza kimya kabisa.
Mnyetishaji wa taarifa hizi aliongea na baadhi ya watumishi na kubainisha kuwa wako tayari kuhamishwa kutoka katika Kituo hicho na kwenda katika Vituo vingine wanakohitaji huduma yao kuliko kuhatarisha maisha yao.
Kufuatia hali hiyo Mh. Nawanda Mkuu wa Wilaya ya Lindi aliwaeleza wananchi hao kwamba kuanzia sasa hataki kusikia tukio hilo likiendelea na ikibainika wanaendelea na mashambulizi hayo kwa watumishi katika siku tatu zijazo, basi atawaondoa kituoni hapo na hataleta mtumishi mwingine na hivyo kituo kitafungwa pamoja na shule ya Msingi.
Post a Comment