
WANACHAMA na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliohusika kwa namna
moja ama nyingine kukihujumu chama hicho wakati wa kampeni za uchaguzi
mkuu na kukikosesha ushindi katika kata na majimbo kadhaa, wametakiwa
kutafuta pa kwenda kabla ya kufukuzwa uanachama.
Kauli hiyo imetolewa juzi na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Tabora Mjini,
Abdulrahman Nkonkota alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara wa wana CCM
kutoka maeneo mbalimbali ya mji huo wa kumpongeza Rais Mteule wa awamu
ya tano, Dk John Magufuli kupitia chama hicho.
Alisema ili CCM iendelee kupata kibali kwa wananchi na kushika dola ipo
haja ya kusafisha chama kwa kuondoa wanafiki na wasaliti walioko ndani
ya chama.
Alisema hao kwa kuwa wanadumaza maendeleo ya chama pamoja na serikali
huku akibainisha wazi kuwa wataanza operesheni safisha chama ili kiweze
kutekeleza malengo yake yapatayo 19.
“Naunga mkono kauli ya Rais wetu Mteule Dk Magufuli ya kuwaondoa
wanafiki katika chama ambao wamerudisha nyuma maendeleo ya chama chetu
hali iliyowafanya baadhi yao kupoteza imani kwa chama chao”, alisema.
Awali Katibu wa CCM wilaya ya Tabora Mjini, Kameth Ndaghine alisoma
tamko la wana CCM wa wilaya hiyo la kumpongeza Dk Magufuli na mgombea
mwenza Samia Suluhu Hassan kwa kuibuka na ushindi wa kishindo katika
uchaguzi mkuu uliofanyika nchini kote Oktoba 25 mwaka huu.
Alisema wanaamini uwezo mkubwa walio nao viongozi hao utawavusha
Watanzania na kuwaondoa katika dimbwi la umasikini sambamba na kuongeza
ajira kwa vijana.
Aidha alimwomba Magufuli mara tu atakapoapishwa ahakikishe anaanza
kutekeleza ahadi zake hasa kwa kujenga mahakama ya mafisadi na
kuwachukulia hatua kali wala rushwa ambao wamelifikisha taifa pabaya.
Ndaghine alisema pamoja na kuanzisha mahakama ya mafisadi awashughulikie
watumishi wa umma wanaoendekeza uzembe na wale wanaofanya kazi kwa
mazoea ili kurudisha imani kwa Watanzania waliomwamini na kuiamini CCM
hadi kuipa ushindi wa kishindo.
Post a Comment