1.0 Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA)
1.1 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, ametengua uteuzi wa Bwana Dickson E. MAIMU, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa kuanzia leo, tarehe 25 Januari, 2016.
1.2 Aidha, baada ya utenguzi huo, Bwana Dickson E. MAIMU amesimamishwa kazi kupisha uchunguzi, pamoja na wafuatao:
1.2.1 Bwana Joseph MAKANI, Mkurugenzi wa TEHAMA
1.2.2. Bi Rahel MAPANDE, Afisa Ugavi Mkuu
1.2.3 Bi Sabrina NYONI, Mkurugenzi wa Sheria
1.2.4 Bwana George NTALIMA, Afisa usafirishaji
1.3 Taarifa zilizomfikia Rais zinaonesha
kuwa NIDA hadi sasa imetumia Sh.179.6 bilioni. Kiasi hiki ni kikubwa na
Rais angependa ufanyike uchunguzi na ukaguzi jinsi fedha hizi
zilivyotumika, maana Rais amekuwa akipokea malalamiko ya wananchi
kuhusiana na kasi ndogo ya utoaji wa Vitambulisho vya Taifa.
1.4 Hivyo, Rais ameelekeza Mamlaka ya
Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) wafanye ukaguzi maalum wa manunuzi
yote yaliyofanywa na NIDA.
1.5 Rais pia ameelekeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali afanye ukaguzi maalum wa hesabu za NIDA, ikiwemo ukaguzi wa “value for money” baada ya kuthibitisha idadi halisi ya vitambulisho vilivyotolewa hadi sasa.
1.6 Rais vile vile ameelekeza Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa ifanye uchunguzi kujiridhisha kama
kulikuwa na vitendo vya rushwa au la.
2.0 Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa
2.1 Aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwenye Serikali ya Awamu ya Nne, Mhe. Mahadhi Juma MAALIM ameteuliwa
kuwa Balozi wa kwanza wa Tanzania nchini Kuwait, kufuatia uamuzi wa
Serikali kufungua Ofisi ya Ubalozi katika nchi hiyo rafiki.
2.2 Rais ameagiza Wizara ya Mambo
ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kianda na Kimataifa
kuwarejesha nyumbani mara moja Mabalozi wawili ambao mikataba yao
imeisha. Leo hii Mabalozi hao wanatakiwa kukabidhi kazi kwa Afisa Mkuu
au Mwandamizi aliye chini yao. Mabalozi hao ni:
2.2.1 Bi Batilda Salha BURIANI, aliyeko Tokyo, Japan
2. 2.2 Dkt. James Alex MSEKELA, aliyeko Rome, Italia.
2.3 Rais amemrejesha nyumbani Balozi wa Tanzania aliyeko London, Uingereza, Bwana Peter Allan KALLAGHE. Anarejea Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa atakapopangiwa kazi nyingine.
2.4 Kwa maana hiyo, vituo vya Ubalozi vifuatavyo viko wazi:
2.4.1 London, kufuatia kurejea nchini kwa Balozi Peter A. KALLAGHE
2.4.2 Brussels, kufuatia aliyekuwa Balozi, Dkt. Deodorous KAMALA kuchaguliwa kuwa Mbunge.
2.4.3 Rome, Italia, kufuatia kuisha kwa mkataba wa Dkt. James Alex MSEKELA.
2.4.4 Tokyo, Japan, kufuatia kuisha kwa mkataba wa Bibi Batilda BURIANI
2.4.5 Kuala Lumpar, Malaysia, kufuatia aliyekuwa Balozi, Dkt. Aziz Ponray MLIMA, kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa.
2.4.6 Brasilia, Brazil, kufuatia kustaafu kwa aliyekuwa Balozi, Bwana Francis MALAMBUGI.
3.0 Tawala za Mikoa
3.1 Rais ametengua uteuzi wa Eng. Madeni Juma KIPANDE kabla hajathibitishwa kwenye cheo cha Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi kutokana na utendaji kazi usioridhisha.
4.0 Utumishi wa Umma
3.2 Nachukua nafasi hii kuwahimiza
viongozi wote katika Utumishi wa Umma, na watumishi wote wa umma,
kubadilika kwa dhati kwenye utendaji wao na uadilifu wao.
3.3 Napenda kusisitiza kuwa Rais na sisi
tunaomsaidia hatuoni raha kuchukua hatua dhidi ya viongozi na watumishi
wengine. Tungependa kila mtu mwenyewe ajirekebishe na kutomfikisha Rais
mahali ambapo inabidi amchukulie hatua. Mambo yafuatayo ni muhimu:
4.2.1 Kila kiongozi na kila mamlaka ya nidhamu isipate kigugumizi kusimamia utendaji na maadili ya kazi.
4.2.2
Kila kiongozi na kila mamlaka ya nidhamu asipate kigugumizi kuchukua
hatua za nidhamu, lakini afanye hivyo kwa kuzingatia kwa ukamilifu
sheria, kanuni na taratibu katika Utumishi wa Umma.
4.2.3 Lazima uongozi na watumishi wa umma wawahudumie wananchi kwa haki, weledi, uadilifu na heshima. Kwa sababu hiyo:
a) Kila ofisi ya Serikali iwe na dawati la kusikiliza shida za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.
b) Kwenye kila Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Ofisi ya Mkuu wa
Wilaya wajenge uwezo wa kushughulikia shida za wananchi kwa ukamilifu na
kwa wakati. Kwa muundo wa Serikali yetu hakuna sababu kwa mwananchi
kufunga safari mpaka Ikulu Dar es Salaam kwa kuamini kuwa ni Rais tu
anayeweza kumaliza matatizo yake, maana wawakilishi wa Rais wako kila
pembe ya nchi yetu. Ikibidi wananchi wafike Ikulu ina maana hao
wawakilishi wa Rais hawakutimiza wajibu wao.
c) Kuanzia sasa watumishi wote wa umma wavae majina yao
ili iwe rahisi kwa mwananchi kumtambua anayemhudumia na hivyo kumsifu
mtumishi wa umma anayewahudumia kwa weledi, uaminifu na kwa wakati, na
kumtolea taarifa yule anayefanya mambo ya hovyo.
d)
Kila ofisi ya Serikali iwe na utaratibu wa kupokea maoni ya wananchi
kuhusu huduma inayotolewa kwenye ofisi hizo, na kushughulikia haraka
maeneo yote ambayo wananchi wataonesha kutoridhika na huduma.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Arusha
25 Januari, 2016
Post a Comment