Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala(KIU)
Mgomo wa wanafunzi wa vitivo vya Sayansi ya Afya vya Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala(KIU)- tawi la Dar es Salaam, umesababisha chuo hicho kufungwa.
Mgomo huo uliokwenda sambamba na maandamano ya wanafunzi, ulisababisha Polisi kuingilia kati na kupambana na wanafunzi hao na baadaye uongozi wa chuo kikifunga kwa muda usiojulikana.
Wanafunzi hao waligoma kufanya mitihani kutokana na uongozi wa chuo kushindwa kushughulikia usajili wa kozi za famasia, maabara na udaktari.
Mmoja wa wanafunzi wa shahada ya udaktari mwaka wa pili, alisema wameamua kugomea mitihani kutokana na kutojua hatma ya kozi wanayosoma kama imesajiliwa hivyo kuushinikiza uongozi kuhakikisha kozi hizo zinafanyiwa usajili.
“Uongozi umekuwa ukitupa ahadi ya kushughulikia madai yetu kwa muda mrefu, cha kushangaza hadi sasa hakuna majibu ya kuridhisha juu ya usajili wa kozi zetu,” alisema.
Aidha, alisema uongozi wa chuo umeshindwa kuwatatulia matatizo hali inayosababisha migomo isiyokwisha.
Naye, mwanafunzi wa Shahada ya Famasia mwaka wa pili, alisema tangu Baraza la Famasia liwape siku 10 kusajili kozi hadi leo kozi yao haijafanyiwa usajili.
Rais wa KIU, Elias Mbogho, alisema wanafunzi wachache wa kozi ya Famasia ndiyo wanawashawishi wenzao kugomea mitihani akisisitiza usaili wa kozi hiyo umefikia katika hatua nzuri.
“Mgomo unaofanyika hauwahusishi wanafunzi wote wa vitivo vya Sayansi ya Afya, bali wanafunzi wa famasia wanachochea mgomo,” alisema.
Kwa mujibu wa Afisa Masoko na Mahusiano wa chuo hicho, Kenneth Uki, kutokana mgomo huo wanafunzi wanne walijeruhiwa na kutibiwa katika zahanati ya KIU kufuatia vurugu zilizozuka juzi chuoni hapo.
Uki, alisema mgomo huo ulisababisha uharibifu wa milango minne na madirisha 75 ambayo hadi sasa thamani yake haijajulikana.
Alisema wanafunzi wanane walikamatwa na polisi na kupelekwa katika Kituo cha Polisi Stakishari-Ukonga.
Aliongeza kuwa uongozi wa KIU umelazimika kufunga vitivo vya masomo ya sayansi kwa muda usiojulikana.
Post a Comment