Haruni Sanchawa
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete ‘JK’, leo katika Viwanja vya Chuo cha Magereza ya Ukonga jijini Dar, ana ratiba ya kuzungumza na maafande na maafisa wa jeshi la magereza na wafungwa katika Siku ya Magereza Tanzania 2015 ambayo huadhimishwa kila mwaka.
Kwa mujibu wa chanzo cha ndani ya jeshi hilo, pia Rais Kikwete atatumia nafasi hiyo kuliaga jeshi hilo kwa vile Oktoba, mwaka huu, nchi itamchagua rais atakayepokea kijiti chake cha urais kwa awamu ya tano.
Msingi wa habari hii ni wafungwa wanaotumikia kifungo cha maisha jela kwa makosa ya ulawiti na ubakaji, wanamuziki Nguza Vicking ‘Babu Seya’ na mwanaye, Johnson Nguza ‘Papii Kocha’ kwani katika hafla kama hiyo, mwaka jana, walimtumia salamu JK wakimwomba awasamehe kwani walishatambua makosa yao.
Risasi Jumamosi: “Je, rais hawezi kuitumia nafasi hiyo kuwaachia huru wanamuziki, Nguza Vicking na mwanaye, ‘Papii Kocha’ ambao wanatumikia kifungo cha maisha jela?”
Chanzo: “Mh! Sina hakika sana. Maana kama hilo lipo ina maana ni jukumu la rais mwenyewe na mipango yake kwa mujibu wa katiba, rais ana mamlaka ya kumsamehe mfungwa kwa kosa lolote lile.”
KUHUSU WARAKA
Risasi Jumamosi: “Juni mwaka jana wakati wa maadhimisho kama hayo, mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe, Babu Seya na Papii walimuomba Rais Kikwete awasamehe kwa makosa waliyofanya ambapo waziri, katika kuwajibu alisema mtu akishatumikia kifungo kwa miaka saba au 10 gerezani ana hakika kama ana moyo na nafasi ya kuacha, atakuwa amebadilika hivyo anaweza kupewa msamaha. Je, rais hawezi kutumia mwanya huo?”
Chanzo: “Sijui. Unajua haya mambo ya msamaha ni ya kiitifaki zaidi. Hawezi kila mtu kujua zaidi ya yeye anayekusudia kusamehe.”
JK, BABU SEYA KUONANA
Kwa mujibu wa chanzo kingine, JK anaweza kuonana na Babu Seya moja kwa moja kwani huenda wafungwa hao watatumbuiza kwenye hafla hiyo kama ilivyokuwa mwaka jana ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri Chikawe.
VIONGOZI WA MAGEREZA WANENA
Baada ya kunyetishiwa hayo na chanzo chetu hicho, Risasi Jumamosi lilimtafuta Afisa Habari wa Jeshi la Magereza Makao Makuu Tanzania, ASP Lucas Mbonje na kumuuliza kuhusu JK kufika kwenye Gereza la Ukonga leo na kuaga jeshi hilo na kuonana na wafungwa, akiwemo Babu Seya na mwanaye, Papii Kocha ambapo alisema:
“Mimi nipo safarini, hiyo ziara ya rais naijua, ni kwenye Siku ya Magereza, lakini mpigie mrakibu wa magereza, anaitwa SP Edwin Kisiluka.”
MRAKIBU SASA
Risasi Jumamosi lilimtafuta mrakibu huyo na kuzungumza naye kuhusu uwepo wa Rais Kikwete kwenye sherehe ya Siku ya Magereza ambapo alisema:
“Ni kweli, kwa ratiba yetu, Rais Kikwete ndiye mgeni rasmi. Tutakuwa naye. Mbali na hilo, Magereza Day kuna maafisa wa cheo cha inspekta watapandishwa vyeo na kuwa ma-ASP.”
“Vipi, unajua lolote kuhusu rais kuitumia nafasi hiyo kuwaachia huru Babu Seya na mwanaye?”
Mrakibu: “Hilo silijui mimi. Ila ratiba ya shughuli yetu ni hiyo niliyokupa.”
WAKATI HUOHUO
Hali ya kiafya ya Papii Kocha inadaiwa kwenda halijojo gerezani humo akiwa anasumbuliwa na ugonjwa wa kifua.
Kwa mujibu wa chanzo, Papii alianza kuumwa mwanzoni mwa mwaka huu hivyo kudhoofika sana na mpaka sasa anaendelea na matibabu.
“Jamani mimi nilikuwa kule kwa miaka kadhaa. Yaani nilifungwa. Papii Kocha anaumwa kifua. Amedhoofika sana. Lakini bado anaendelea na matibabu,” kilisema chanzo hicho hivi karibuni.
Babu Seya na Papii walihukumiwa kifungo cha maisha mwaka 2004 hivyo mwaka huu wametimiza miaka 11 jela.
-CHANZO: Globalpublishers
-CHANZO: Globalpublishers
Post a Comment