Msanii wa kike wa muziki wa Bongo Fleva nchini, Diana Malaika Exavery Clavery 'Malaika',akiwa katika pozi wakati wa mahojiano na Global TV Online leo....Akiimba wimbo wake wa Sare aliomshirikisha Mesen Selekta.
(PICHA: BRIGHTON MASALU/GLOBAL TV ONLINE)
UMESHAMSIKIA na pengine umeshamuona kwenye video, lakini mtandao namba moja wa Global Publishers unakuwa wa kwanza kumuweka sura yake na maongezi yake kifaa kipya kwenye muziki wa Bongo Fleva.
Ukisikia kiitikio cha Wimbo wa Uswazi Take Away wa Said Nassor ‘Chegge’ lazima utajiuliza mara mbilimbili sauti ya kike inayosikika ni ya nani.
Jibu ni rahisi! Ni mmoja kati ya wasanii wa kike wasioshikika katika Bongo Fleva kutokana na staili yao ya kuimba na kucheza. Anaitwa Diana Malaika Exavery Clavery ama wengi wamezoea kumuita Malaika.
Ukiachana na Uswazi Take Away, Malaika anatambulika na ngoma kama Mwantumu, Nenda pamoja na Saresare aliyomshirikisha prodyuza, Mesen Selekta wa De Fatality Music.
Ikumbukwe kuwa pia katika hafla fupi ya utoaji tuzo za Kili Music mwaka 2015, Malaika alikuwa mmoja wapo katika vipengele vya tuzo hizo akichuana na Lady Jay Dee, Linah, Grace Matata pamoja na Vannesa Mdee akiwania kipengele cha Mwimbaji Bora wa Kike Bongo Fleva ambapo tuzo ilikwenda kwa mwanadada, Vannesa Mdee.
Mapema wiki hii nilikutana na Malaika kisha akafunguka mengi kuhusiana na maisha yake kimuziki na katika makala haya yanaweka wazi;
Ulikutana wapi na Chegge?
(Anacheka kidogo...)
Nilikuwa nasoma shule ya wasichana ya Kibosho huko Moshi. Nilipomaliza kidato cha nne nikaingia jijini Dar na kufanya ‘field’ kwenye Ofisi za Uzazi na Vifo (RITA) na wakati mwingine nilikuwa nafanya kazi kwa mtayarishaji wa video, Adam Juma wa Visual Lab kama ‘make up artist.’
(Anashusha pumzi kidogo kisha anaendelea...)
Kitendo cha kuwa na Adam kwa muda mrefu na wasanii wengi wanakuja pale, basi ikawa rahisi kwa Adam kuniunganisha na Chegge na kweli alisikia tu sauti yangu moja kwa moja akanikubali na ndiyo kama unavyosikia kwenye Wimbo wa Uswazi Take Away nilivyotendea haki kiitikio.
Wasanii wangapi umeshawafanyia make up?
(Anacheka...)
Kwakweli mpaka sasa siwezi kutaja orodha yake juujuu kwani ni wasanii wengi sana ambao walikuwa wakija kwa Adam kutengenezewa video kisha wanapitia mikononi mwangu, bali ninaowakumbuka ni Diamond, Dully, Ommy Dimpoz, Queen Darlin pamoja na Keisha.
Mpaka sasa una ngoma ngapi?
(Anatingisha miguu yake huku kichwa kikiwa juu...)
Sina ngoma nyingi kwakuwa kwenye gemu la muziki nipo kwa muda mfupi japokuwa nimekuja kwa kasi sana. Nina nyimbo tatu na ya kwanza inaitwa Nenda ambayo ilivuja.
Ya pili ni Mwantumu iliyopokelewa vema na watu wazima na wa mwisho ni Saresare unaoimbwa hadi na watoto.
Changamoto kwenye muziki?
(Anatingisha kichwa kwa masikitiko...)
Muziki wangu najisimamia mwenyewe hapohapo najihusisha na biashara za magari kwahiyo kichwa hichohicho kinakuwa kikiwafikiria mashabiki utokaje, uwaburudishe vipi na muda mwingine biashara.
(Anafikiria huku akichezesha mikono...)
Halafu kikubwa naweza kusema nina bahati, katika historia yangu sijawahi kutongozwa sasa sijui ndiyo naogopwa
(Anacheka kwa sauti ya juu huku kichwa akikielekezea chini...)
Nyimbo zako nani anakutungia?
(Anashtuka...)
Mimi? Wala situngiwi na mtu yoyote. Tukianzia Wimbo wa Nenda nilitunga mwenyewe, Mwantumu nao mwenyewe na huu wa sasa hivi wa Saresare nimeutunga mwenyewe ila kuna vionjo f’lani ameongezea Mesen.
Kwanini wasanii wa kike Bongo hamna ushirikiano?
(Simu yake inaita, anapokea na kuongea, kisha anamaliza na kukata...)
Sorry...
Ujue sisi ngozi nyeusi kwa upande wa wanawake tuna uoga tangu zamani. Wasichana wenyewe kwa wenyewe tunajiogopa.
Muziki umekuletea mafanikio yoyote?
(Anashtuka tena, anataka kupokea simu lakini anaamua kuikata...)
Muziki umeniletea mafanikio mengi kwa kipindi kifupi, kwanza nimeweza kuingiza pesa kwa muda mfupi.
Pili katika uzinduzi wa Wimbo wa Mwantumu niliweka rekodi ya aina yake pale Maisha Club kwa kujaza ukumbi hadi uongozi haukuamini.
Tatu muziki umeniletea kujuana na watu, nilishawahi kuitwa Ubalozi wa Europe kupiga shoo katika siku yao ya kitaifa ambapo walinipa mashairi ya wimbo wao wa taifa na kunitaka niimbe nikafanya hivyo.
Usiku huo uliniwezesha kukutana na wasanii wengi wa kimataifa na wakakubali kazi zangu
Post a Comment