Hali hiyo ndani ya Bunge iliendelea kwa siku ya pili mfululizo na mara zote kusababisha Spika kuahirisha vikao baada ya shughuli za Bunge kushindwa kuendelea kutokana na kelele za wapinzani wanaopinga kitendo cha uongozi kuwasilisha miswada mitatu kwa hati ya dharura wakidai hakuna haja ya haraka hiyo.
Jana Spika Makinda, ambaye aliwahi kukumbana na hali kama hiyo wakati wa mjadala wa sakata la Akaunti ya Escrow kwenye Bunge la 18, aliibuka na dawa mpya na kuitumia Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuwaadhibu wabunge hao saba.
John Mnyika, Moses Machali, Tundu Lissu, Felix Mkosamali na Paulin Gekul, ambao wamekuwa wakipinga hoja mbalimbali za Serikali ikiwa ni pamoja na miswada mitatu iliyotakiwa kuwasilishwa kwa dharura kuanzia jana, wamefungiwa kushiriki vikao kuanzia leo hadi Bunge litakapovunjwa Julai 9.
Wabunge wengine wawili, Mchungaji Peter Msigwa na Rajab Mbarouk wamefungiwa kushiriki vikao viwili kuanzia leo baada ya Kamati hiyo kuwatia hatiani wawakilishi hao wote saba kwa kudharau mamlaka ya Spika.
Wengine watatu, Joseph Selasini, Khalifa Suleiman Khalifa na Rajabu Abdalah wanatakiwa kufika mbele ya kamati hiyo leo saa 4:00 baada ya wito wa kuwataka wahudhurie jana kuchelewa.
Kikao cha jioni cha Bunge hilo, ambacho kilipokea taarifa ya kamati hiyo ya maadili na mapendekezo ya adhabu hizo, kilichelewa kuanza kwa saa moja na dakika ishirini kusubiri kumalizika kwa kazi ya kuwahoji watuhumiwa.
“Mashtaka yetu yaliendeshwa kwa haraka, hatukupatiwa muda wa kutosha kujieleza wala kumtumia wakili,” alisema Machali baada ya Bunge kuahirishwa.
“Pamoja na kuadhibiwa, hatutaogopa kusema kuwa miswada hiyo ina matatizo ili Watanzania wafahamu na iwapo miswada hiyo itapitishwa malalamiko ya vizazi vijavyo juu yatakayotokea kwenye sekta ya gesi yatakuwa juu ya Serikali na CCM.”
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alisema ni bora kufukuzwa kuliko kuendelea kushuhudia gesi ya Watanzania ikiuzwa kwa nguvu bila ya huruma.
“Hii ni bora kuondolewa. Hukumu haikuwa ya haki na tungeweza kukata kukata rufaa kwenye Kamati ya Kanuni, lakini mwenyekiti wake ni Spika hivyo basi tena, acheni wafanye wanachotaka kukifanya,” alisema Lissu.
Mchungaji Msigwa, ambaye ni mbunge wa Iringa Mjini, alisema hata angefungiwa kushiriki vikao vyote, asingeathirika.
Post a Comment