Baada ya kuona kwa siku nne mfululizo nina kuwa na ndoto inajirudia, nimeona nitafute msaada wa kitaalamu. Kila ikifika saa nane ya usiku ndoto ya kutisha inaanza, najiona nimeshashinda uchaguzi na nimechaguliwa kuwa rais, magazeti na mativi yote yananishangilia, wananchi wenye furaha wako mitaani na mabango yenye jina langu, mipango yote ya kuniapisha inaanza, umeme unakatika wapambe wanajitahidi kurudisha umeme inashindikana halafu inatangazwa kuwa wataniapisha kesho yake nashtuka najikuta peke yangu ndani ya geto langu, mwili umelowa jasho natetemeka kwa woga, na ndiyo sipati usingizi tena.
Hivyo nimeona nione wataalamu kuhusu hili, siyo wale wataalamu wenu wanaobandika matanganzo kwenye nguzo za umeme hapana, nimeenda kwenye hospitali moja jirani, nipime malaria kwanza, maana ndoto nyingine ni dalili ya malaria kupanda kichwani, kwa nini niote nimekuwa rais kama siyo kichaa hicho?
Wakati niko kwenye benchi la mapokezi nasubiri majibu ya vipimo nilivyofanya, ghafla mbaba mmoja alitoka spidi kali toka chumba cha daktari na kutokomea mtaani, nesi aliyekuwa karibu yangu akaanguka kicheko hadi akakaa chini. Nikaanza kumhoji, huku akiwa anacheka akasema, “Sindano hiyo” Sikumuelewa.
Alipotulia ndipo akaanza kueleza kuwa hilo ni tatizo la kawaida sana kuna watu wanaogopa sindano, kwa hiyo hutimka kama wanafukuzwa. Nesi akanitajia jina la baunsa mmoja maarufu ambaye mara nyingi huwa bodi gadi wa masupastaa wetu na ana kawaida ya kuvaa miwani nyeusi hata usiku, huwa sura yake inayoonesha hacheki na mtu, basi nesi akasema jamaa huyo akiambiwa kuwa atachomwa sindano hulainika ghafla kama bamia, hata sauti inakuwa kama mtoto akiomba abadilishiwe matibabu.
Nesi akataja msanii wa muvi mmoja mashuhuri kwa kuekti kama jambazi, basi huyu hulia kama mtoto mdogo anapochomwa sindano. Bila kupepesa macho nesi akanitaarifu kuwa hata mjumbe wa serikali ya mtaa wangu naye akisikia sindano machozi humlengalenga na bila kukamatwa hutimka mapema.
Pamoja na kuwa wakati huo na mimi nilishiriki kucheka habari hizi za kudhalilisha, lakini sikuwa na raha maana majibu yangu yalikuwa hayajatoka. Kimoyomoyo nikawa najiuliza, je, na mimi nikiambiwa lazima nichomwe sindano itakuwaje? Kwa kweli patachimbika, maana hapa nilipo nina jino linanisumbua karibu miezi sita, nimeshaambiwa dawa ni kung’oa, lakini kila nikiwaza ile ishu ya kuchomwa sindano mdomoni naishia kumumunya panado na karafuu kupunguza maumivu.
Najua wazungu wameshagundua vidonge vingi, sasa kwa nini madaktari wanang’ang’ania kuchoma sindano tu? Au wanaona raha sana kutuona wakubwa wazima tunatetemeka? Muda si mrefu dokta akaniita na kuniambia nina malaria, hivyo nijipange kuchomwa sindano za masaa. Nilimcheki dokta nikagundua muonekano wake unaonesha kazi hii hana uzoefu nayo, nikaamua palepale kuwa naenda kupata dawa mbadala.
Palepale nikamwambia, “ Dokta sawa ila naomba niende nyumbani kidogo nikirudi ndiyo anichome sindano’ Akaanza ubishi eti anataka lazima nichome ndiyo niendelee na shughuli zangu. Kwa kweli siyo siri hawa ndiyo madokta wanaotufanya tukatibiwe kwa Karumanzila, maana kule kamwe hakuna sindano. Niliaga kama nakwenda msalani kufika nje nilitimua mbio kama nafukuza mwizi vile!

Post a Comment