
Zikiwa zimesalia siku nne Uchaguzi Mkuu ufanyike, Rais Jakaya Kikwete amelitaka Jeshi la Polisi nchini kuwa makini na watu aliowataja kuwa chanzo cha kuleta vurugu siku ya kupiga kura, Jumapili hii.
Rais
Kikwete ambaye alilipongeza pia jeshi hilo kwa kusimamia vizuri
mikutano yote ya kampeni tangu ilipoanza, alisema mtihani uliobakia sasa
ni wa kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa amani na usalama.
Kauli
hiyo aliitoa jana katika Viwanja vya Chuo Kikuu cha Polisi Dar es
Salaam, baada ya kupokea magari 399 yatakayotumiwa na jeshi hilo.
Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, magari hayo ni kati ya 777 yaliyonunuliwa na Serikali kutoka India.
“Mmesimamia
vizuri mikutano ya kampeni, ninawapongeza, lakini msionyeshe ulegevu
kwenye hatua ya mwisho iliyo mbele yenu, hakikisheni mnawazuia wote
wanaotaka kuleta vurugu na kuwafanya watu waogope kwenda kupiga kura,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Lakini
sijasema muwaonee watu, badala yake hakikisheni mnakuwa wakali kwa wote
watakaoonyesha dalili za kuvunja sheria. Tunachotaka watu wapige kura
wakiwa katika hali ya utulivu bila hofu.”
Miongoni
mwa magari aliyoyapokea ni malori maalumu kwa ajili ya kazi ya kubebea
askari, magari ya Zimamoto na mengine manane maarufu washawasha kwa
ajili ya kuzuia vurugu.
Hata
hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe alitumia
nafasi hiyo kukanusha uvumi ulioenea mitaani kuwa magari hayo yameletwa
kwa ajili ya kutumika katika kipindi hiki cha uchaguzi.
“Uvumi
huo hauna ukweli, magari haya tumeyaleta kwa ajili ya kuliongezea
ufanisi wa kazi jeshi letu la polisi ambalo kwa muda mrefu limepungukiwa
vitendea kazi yakiwamo magari,” alisema Chikawe.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Rais Kikwete aliyesema:
“Maneno
ni mengi na watu wamezoea kusema, lakini ukweli unabakia kuwa magari
haya yamenunuliwa kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa kazi ndani ya jeshi
letu.”
Wakati
huohuo; Rais Kikwete alisema anaondoka madarakani akiliacha jeshi hilo
likiwa salama na imara licha ya kutokamilisha baadhi ya mahitaji yake
aliyoahidi kulipatia.
“Naondoka jeshi likiwa imara, lakini kuna vitu havijakamilika ila tayari kuna fedha zimeshatengwa kwa ajili hiyo,” alisema Rais Kikwete.
~Mpekuzi blog
Post a Comment