Makarani
na mahakimu wa Mahakama ya Mwanzo ya Morogoro wakifanya usafi katika
ofisi za mahakama hiyo sanjari na kupanga mafaili vizuri.
Dustan Shekidele, MORO
HAPA kazi tu! Zile ziara za kushtukiza (bila
taarifa) zinazofanywa na Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano za
Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli ‘JPM’ zimezua kizaazaa mjini hapa,
hususan katika Mahakama ya Mwanzo ya Morogoro.
Karani akiwa amevalia kanga wakati akiendelea kuweka mambo sawa.
Jumatatu ya wiki hii, paparazi wetu
aliwanasa makarani na mahakimu wa mahakama hiyo wakifanya usafi katika
ofisi za mahakama hiyo sanjari na kupanga mafaili vizuri kwa kile
kilichosemekana kuwa ni tahadhari kabla ya hatari kwa vile uongozi wa
mahakama hiyo ulichezwa na machale ya Rais Magufuli kuwashtukizia.
MAKARANI WAVAA KANGA
Katika safishasafisha hiyo, baadhi ya
makarani walivaa kanga kwa kujifunga juu ya magauni yao kama wapo
majumbani mwao kwa lengo la kujikinga na vumbi la muda mrefu ndani ya
mashelfu ya mafaili mahakamani hapo.

Mafaili ya mahakama hiyo yakiwa yametupwa chini.
Ilionekana kuwa ni jambo la kuhakikisha
kila mfanyakazi anashughulika na zoezi hilo huku wengine wakionekana
kutokunywa hata chai ili zoezi hilo likamilike kwa wakati.
Karani wa mahakama hiyo
aliyejitambulisha kwa jina la Mwajuma Nyundo alipoulizwa na paparazi
wetu kuhusu zoezi la usafi huo, alisema:
“Hapa ni kizaazaa tu! Si unaona kasi ya
Rais Magufuli ya sapraizi akitekeleza kauli mbiu yake ya ‘Hapa Kazi Tu’.
Hivyo katika kutekeleza kauli mbiu hiyo leo viongozi wetu wametupa kazi
hii.”
Akizungumza na gazeti hili kwa sharti la
kutotajwa jina gazetini, mfanyakazi mwingine alisema lengo la kuweka
ofisi katika hali ya usafi ni kuhofia kuumbuka endapo Magufuli atatia
timu ghafla.
MAFAILI YAWEKWA SAWASAWA
“Si unajua Magufuli anavyotikisa nchi
kwa sasa. Yaani huwezi kujua muda wala saa atakayoibukia kwako. Tumeamua
kufanya usafi ili mahakama iwe safi.
“Sasa hivi hata zile kesi za muda mrefu
tunapanga mafaili upya, yakae mbelembele na kuweka lebo ya kutamabulisha
kesi ili mashauri hayo yaendelee na kumalizika kwa wakati,” alisema
mfanyakazi huyo huku akiendelea na shughuli zake.
Mfanyakazi mwingine naye alisema:
“Tunatekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya Rais Magufuli ya ‘Hapa Kazi Tu’
ili akifanya ziara ya ghafla katika mahakama yetu atukute tuko vizuri.”
Wakiendelea kupanga mafaili.
IJUMAA LAZUNGUMZA NA HAKIMU
Baada ya kusikia hayo kutoka kwa
wafanyakazi wa mahakama hiyo, paparazi wetu alibisha hodi kwenye mlango
wa chumba cha mashtaka na kuzungumza na kiongozi wa mahakama hiyo,
Mheshimiwa Janne Melle ambapo alipoulizwa alisema:
“Na mimi nimepokea maagizo haya kutoka
Mahakama ya Wilaya. Halafu bwana mwandishi hizo picha ulizopiga naomba
sana ukishazisafisha niletee na mimi nizipeleke wilayani.”
KUMBE SI MAHAKAMANI TU
Ukiachia mahakama hiyo, wafanyakazi
wengi wa ofisi za serikali mkoani hapa wamebadili tabia ambapo sasa, saa
moja asubuhi wapo barabarani kwa lengo la kuwahi muda wa kuingia kazini
ambao ni saa moja na nusu tofauti na zamani ambazo kuchelewa kazini
ilionekana kama fasheni.
WASEMAVYO MOROGORO
Baadhi ya wakazi wa mjini hapa walipoongea na Ijumaa
kuhusu tabia ya Magufuli ya kuzuka maofisini bila taarifa, walipongeza
huku wakisema huyo ndiye rais anayetakiwa kwa sasa hapa Bongo.
“Tabia zetu Wabongo tunataka rais kama
Magufuli. Unajua sisi ni watu wa kusukumwa sana! Sasa tukimpata rais
asiyeweza kusukuma, ndiyo nchi inakwenda mrama. Mimi nampongeza sana
Magufuli.
“Kwa staili hii ya Magufuli ya
kushtukiza ziara ya maeneo mbalimbali watu watanyooka. Kwa wale wavivu
na wazembe makazini lazima waombe po,” alisema Jumanne Kihamba, mkazi wa
Misufini mjini hapa.
GUMZO LA NCHI NI MAGUFULI
Kwa sasa ukiachia vyombo vya habari kama
magazeti, ndani ya mitandao mbalimbali ya kijamii gumzo ni Magufuli.
Hiyo yote ni kufuatia hatua yake ya kufanya ziara za kushtukiza ambapo
tangu aingie madarakani ameshawashtukiza watumishi wa Wizara ya Fedha
(Hazina) na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Kitendo hicho kimeibua mpaka utani
kwenye mitandao ambapo baadhi ya watu wamekuwa wakitunga vituko
mbalimbali kuashiria kwamba, Magufuli ni kiboko ya watendaji wazembe
serikalini.


Post a Comment