Wakati Chama cha Wanasheria wa Zanzibar (ZLS) kikisema kwa mujibu wa
Katiba ya Zanzibar tarehe ya mwisho ya Dk Shein kuingia ofisini ni leo
Novemba 2, polisi kwa upande wao wanasema Rais huyo anatakiwa kushika
madaraka hayo hadi pale rais mpya atakapoapishwa.
Rais wa ZLS, Awadh Ali Said alisema mwishoni mwa wiki kuwa moja ya
athari za tamko la Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kufuta uchaguzi wa
Zanzibar ni kusababisha mgogoro wa kikatiba hasa katika muda wa rais
kushika madaraka.
Said alisema Ibara ya 28 (2) ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 inaeleza kuwa
Rais ataacha madaraka yake baada ya kumalizika miaka mitano kuanzia
tarehe alipokula kiapo cha uaminifu na kiapo cha kuwa Rais.
Alisema tafsiri yake ni kuwa tangu Dk Shein alipokula kiapo cha uaminifu
na kiapo cha kuwa rais Novemba 3, 2010 atakuwa ametimiza miaka mitano
Novemba 2, 2015.
“Hivyo akiendelea kushikilia madaraka ya urais zaidi ya tarehe hiyo itakuwa kinyume na Katiba ya nchi,” alisema.
Kutokana na madai hayo, Jeshi la Polisi Zanzibar limewatahadharisha
wananchi kutojihusisha na vitendo vya fujo kwa madai kwamba kuanzia leo
hakutakuwa na Serikali.
-Mwananchi
-Mwananchi
Post a Comment