Mbunge
wa Kilombero, Peter Elijualikali jana alijikuta akitolewa nje ya kikao
cha Halmashauri ya Kilombero na jeshi la polisi kwa amri ya Mwenyekiti
wa kikao hicho kwa madai kuwa sio mjumbe halali wa kikao hicho, hivyo
haruhusiwi kupiga kura kumchagua Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo.
Sintofahamu
hiyo iliibuka wakati Halmashauri hiyo ikijipanga kufanya uchaguzi wa
Mwenyekiti wake, ambapo Mwenyekiti wa kikao alimtaka mbunge huyo kutoka
nje kwa madai kuwa sio mjumbe halali na alipogomea agizo la mwenyekiti,
aliondolewa nje kwa nguvu na polisi.
Mwenyekiti
wa kikao hicho alieleza kuwa wamepokea ufafanuzi kutoka TAMISEMI kuwa
mbunge huyo wa Kilombero anapaswa kuwa mjumbe wa vikao vya Halmashauri
mpya ya Ifakara na sio halmashauri ya Kilombero.
Hata
hivyo, maelekezo hayo yalipingwa vikali na madiwani wa vyama vya
upinzani vinavyounda Ukawa pamoja na mbunge huyo ambaye alieleza kuwa
amepanga kwenda mahakamani kudai haki yake.
“Waziri
wa TAMISEMI kama hataki kuchafuka na Katibu Mkuu wake, naomba wafanye
kila wanaloliweza nirudi kwenye Halmashauri yangu. Na wasipofanya hivyo,
nakwenda Mahakamani,” alisema Elijualikali.
Hatua
hiyo ya kumtoa mbunge huyo na kumuelekeza kuhudhuria vikao vya
halmashauri ya mji wa Ifakara ilitafsiriwa na madiwani wa Ukawa kuwa ni
mbinu ya kutaka kupunguza idadi ya wajumbe wa vyama hivyo ili kuwezesha
CCM kushinda nafasi ya Umeya wa Halmashauri hiyo.
Idadi
ya wajumbe halali wa Ukawa ni 19 huku wa CCM wakiwa 18. Hata hivyo,
Halmashauri ya Ifakala haina Mbunge kwakuwa sio jimbo. Hivyo, hiyo ni
sababu ya kumuelekeza Mbunge huyo kuwa sehemu ya Halmashauri hiyo.
Post a Comment