Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amempongeza
Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuteuliwa
na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mheshimiwa Ban Ki-moon kuunda jopo la
watu mashuhuri watakaomshauri juu ya namna bora ya kuendeleza na
kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu hususani katika afya ya uzazi
ya Mama na mtoto.
Jopo
hilo la watu mashuhuri linaongozwa na wenyeviti wenza ambao ni Rais wa
Chile Mheshimiwa Michelle Bachelet na Waziri Mkuu wa Ethiopia Mheshimiwa
Hailemariam Desalegn, huku Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete na Rais
Mstaafu wa Finland Mheshimiwa Tarja Halonen wakiteuliwa kuwa wenyeviti
mbadala.
Katika
Pongezi hizo Rais Magufuli amesema kuteuliwa kwa Rais Kikwete kuwa
miongoni mwa jopo la kumshauri Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
kumeijengea heshima Tanzania na kumechochea matumaini ya mafanikio ya
kukabiliana na changamoto za afya ya mama na mtoto hususani kwa nchi
zinazoendelea ikiwemo Tanzania.
Rais
Magufuli ameahidi kuwa serikali yake ya awamu ya tano itatoa
ushirikiano katika kutimiza malengo ya maendeleo endelevu ambayo jopo
hilo litamshauri Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ikiwemo katika
kuimarisha afya ya uzazi wa mama na mtoto.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
25 Januari, 2016
Post a Comment