Wataalam
kutoka Shirika la Umeme (Tanesco) pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa
Nishati na Maji (EWURA), wanaendelea kupiga hesabu kabla ya kuja na
majawabu ya kushusha bei ya umeme.
Aidha,
Profesa Muhongo alisema, kwa mara ya kwanza, wanataka nyaya zote za
umeme jijini Dar es Salaam hususan katikati ya jiji, zipite chini ya
ardhi.
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema jana bungeni
kwamba bei hiyo itashuka kwa mchakato huo (wa kupiga hesabu) na si
kwenye majukwaa.
Alikuwa
akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Vunjo, James Mbatia
(NCCR-Mageuzi) aliyetaka kufahamu hatua ambazo serikali imefikia katika
uzalishaji, usambazaji na umeme kwa ubia.
“Kuhusu
bei ya umeme, wengine wanasema nilisema ishuke haijashuka…nilisema
tunapiga hesabu. Bei huwezi kuongea kwenye majukwaa. Tanesco na Ewura
wanapiga hesabu tunataka kushusha bei na si kwenye majukwaa,” alisema.
Kwa
upande wa nyaya za umeme, alisema mkandarasi ameelekezwa ifikapo Aprili
mwaka huu, serikali iachane na kesi za nyaya kuanguka kwa kuwa zitakuwa
zimepitishwa chini ya ardhi.
“Kwa
mara ya kwanza, Serikali inataka nyaya zote za umeme zipite chini ya
ardhi,” alisema na kufahamisha bunge kwamba, maeneo ya Mbagala na
Temeke, inajengwa transfoma kubwa.
Pia kwa upande wa Jimbo la Kibamba, inaondolewa transfoma yenye kilovolti 100 a kuwa na yenye kilovolti 2000.
Alisema
Tanzania ijayo itakuwa ya umeme mwingi na wa bei nafuu ambapo
inatarajia kuwa na umeme wa megawati 10,000. Profesa Muhongo alisema
serikali inaendelea kukaribisha wawekezaji na kwamba Tanzania ijayo
itakuwa ya umeme mwingi na wa bei nafuu.
Akizungumzia
suala la usambazaji umeme, alisema kuna miradi kadhaa inaendelea
kutekelezwa na serikali kwenye maeneo mbalimbali nchini. Profesa Muhongo
alisema umeme uliopo hivi sasa hauvuki megawati 1,500 na ili kufikia
lengo wanahitaji kufikia megawati 10,000.
Awali
akijibu swali la msingi la Mbunge wa Kibamba, John Mnyika (CHADEMA),
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani, alisema ukarabati
wa miundombinu katika jimbo hilo, unatarajiwa kuanza wakati wowote
kuanzia mwanzoni mwa mwezi ujao na kukamilika Juni, mwaka huu.
Post a Comment