Wafanyakazi
saba kati ya wanane wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA)
waliotuhumiwa kuhusika kutorosha makontena 11,019 na magari 2,019 kutoka
bandarini ambao walitoroka, wamepatikana na tayari wanaendelea kuhojiwa
na polisi juu ya tuhuma hizo.
Watumishi
hao ni kati ya watuhumiwa 15 wa TPA waliotangazwa na Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa kuwa wameshiriki
kuondosha makontena na magari hayo kutoka katika bandari kavu saba bila
kulipa ushuru wa Bandari.
Meneja
Mawasiliano wa TPA, Janet Ruzangi alisema jana kuwa mfanyakazi mmoja
kati ya hao wanane, hajapatikana; na anaendelea kusakwa na polisi ili
afikishwe kwenye vyombo vya sheria.
“Wote
walishapatikana kasoro mtumishi mmoja, Happygod Naftali, ambaye huyu
alishaacha kazi siku nyingi baada ya viongozi kuanza kufuatilia suala
hilo; lakini bado polisi wanaendelea kumsaka,” alisema Ruzangi.
Mkuu
wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alithibitisha
watuhumiwa hao, kukamatwa na kwamba bado wanaendelea kuhojiwa kuhusu
tuhuma hizo.
“Ni kwamba tunaendelea na upelelezi wetu,” alisema Sirro licha ya kuwa hakutaka kutaja idadi ya wafanyakazi wa TPA ambao wamepatikana. “Kwa kweli idadi nitaitoa siku nitakapozungumza na waandishi wa habari wiki hii,” alifafanua.
Watumishi
waliokuwa wanasakwa na polisi waliopatikana kwa mujibu wa Ruzangi ni
Aron Lusingu, Amani Kazumari, John Mushi, Valentine Sangawe, Bonasweet
Kimaina, Zainab Bwijo na Nathan Edward.
Watumishi
hao wanaungana na watumishi wengine saba John Elisante, Leticia Masaro,
Christina Temu, Merina Chawala, Adnan Ally, Masoud Seleman na Benadeta
Sangawe waliokamatwa na kuhojiwa kuhusu sakata hilo. Watumishi hao saba,
kwa mujibu wa Sirro, tayari walishapelekwa mahakamani.
“Ukiacha wale saba ambao tumeshawafikisha mahakamani, hawa wengine bado tuko nao tunaendelea kufanya upelelezi,” alieleza.
Wafanyakazi
hao wanatuhumiwa kuhusika kutorosha makontena 11,884 na magari 2,019
ambayo yalitoroshwa kutoka katika Bandari Kavu (ICD) saba bila kulipiwa
ushuru wa bandari na hivyo kuipotezea Serikali mapato ya Sh bilioni
48.55.
Kuhusu
mawakala 280 waliopewa siku saba wawe wamewasilisha maelezo yao makao
makuu ya TPA namna ya walivyohusika kulipia makontena hayo, Ruzangi
alisema mamlaka yake inajipanga kutoa taarifa kamili juu ya suala hilo.
“Tunaendelea kuandaa taarifa ya kilichotokea na kilichobainika kuhusu mawakala hao, tutatoa taarifa hivi karibuni,” alisema Meneja Mawasiliano huyo.
Tangu
Rais John Magufuli aingie madarakani, uongozi wake umeibua ufisadi wa
kutisha ambao ulikuwa unafanywa Bandari ya Dar es Salaama kwa
kuwashirikisha wafanyakazi wa TPA na mawakala pamoja na wafanyakazi wa
Mamlaka ya Mapato (TRA).
Kwa
mara ya kwanza upotevu wa makontena 349 uligundulika baada ya Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa kutinga bandarini na kubaini makontena hayo
kutolewa bandari kavu bila kulipiwa kodi.
Upotevu
huo ulifanya vigogo wa TRA, akiwemo Kamishna Mkuu Rished Bade na
makamishna wengine kusimamishwa kazi na kufikishwa mahakamani.
Baadaye Majaliwa alibaini upotevu wa makontena 2,431 yaliyoondolewa bandari kavu bila kulipiwa ushuru wa Bandari.
Katika
sakata hilo, baadhi ya mawakala wa forodha walifungiwa kufanya biashara
na TPA Sakata la mwisho ni la kupotea kwa makontena 11,019 na magari
2,019, ambayo yaliondolewa kwenye ICD saba bila kulipiwa ushuru wa
bandari na kuipotezea serikali mapato ya Sh bilioni 48.
Post a Comment