Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amelaani
kitendo cha watu wanaosadikiwa kuwa ni majangili kumuua kwa kumpiga
risasi Rubani wa helkopta Kepteni Roger Gower, raia wa Uingereza na
kisha kuidondosha helkopta aliyokuwa akiiendesha wakati alipoungana na
Askari wa wanyamapori waliokuwa wakikabiliana na majangili katika pori
la akiba lililopo katika wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu.
Rais
Magufuli ameelezea kusikitishwa sana na tukio hilo na ameitaka Wizara
ya Maliasili na Utalii kuhakikisha waliomuua Kepteni Gower na
kuidondosha helkopta aliyokuwa akiiendesha wanakamatwa na wanafikishwa
mikononi mwa vyombo vya sheria.
Amemtumia
salamu za pole, Balozi wa Uingereza hapa nchini kwa kumpoteza raia wake
ambaye alikuwa akitoa mchango mkubwa katika kuhifadhi wanyamapori wa
hapa nchini Tanzania.
Aidha,
Rais Magufuli amesema serikali yake itahakikisha inaendeleza mapambano
dhidi ya ujangili kwa nguvu zake zote na kuwataka wananchi na wadau
mbalimbali wa hifadhi ya wanyamapori, kutokatishwa tamaa na tukio hili
na watoe ushirikiano wa kutosha kuwafichua watu wote wanaojihusisha na
ujangili ama biashara ya bidhaa zitokanazo na ujangili.
Katika
tukio hilo, pamoja na kumuua Kepteni Roger Gower watu hao wanaosadikiwa
kuwa majangili wamemjeruhi Askari wanyama pori mmoja na wamewaua tembo
watatu.
Gerson Msigwa.
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU.
Dar es salaam
31 Januari, 2016
Post a Comment