Katibu
Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue ameagiza na kusisitiza ofisi zote
Umma kusimamia na kuhakikisha kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Machi
mwaka huu kila watumishi awe na kitambulisho (beji) kinachoonesha jina
lake.
Akiongea
na waandishi wa habari jijini Dar es salaam Balozi Sefue alisema hatua
hiyo ya watumishi wa umma kuvaa beji zenye majina kila wakati
wanapotekeleza majukumu yao itasaidia wananchi kuwatambua kwa majina
watumishi wanaowahudumia na kuwasaidia kulingana na mahitaji yao kwenye
ofisi hizo.
Ili
kutekeleza azma ya kuwahudumia wananchi, Balozi Sefue alisema kuwa
kuanzia sasa watumishi wote wa umma wavae beji zenye majina yao iwe
rahisi kwa mwananchi kumtambua anayemhudumia na hivyo kumsifu mtumishi
wa umma anayewahudumia kwa weledi, uaminifu na kwa wakati na kumtolea
taarifa yule anayefanya mambo ya hovyo.
Zaidi
ya hayo, Balozi Sefue amewahimiza viongozi na watumishi wote katika
Utumishi wa Umma kubadilika kwa dhati kwenye utendaji na uadilifu wao na
kuwahudumia wananchi kwa haki, weledi, uadilifu na heshima.
“Rais
na sisi wote tunaomsaidia hatuoni raha kuchukua hatua dhidi ya viongozi
na watumishi wengine, tungependa kila mtu mwenyewe ajirekebishe na
kutomfikisha Rais mahali ambapo inabidi amchukulie hatua” alisema Sefue.
Mambo
muhimu yanayopaswa kuzingatiwa ni pamoja na kila kiongozi na mamlaka ya
nidhamu isipate kigugumizi kusimamia utendaji na maadili ya kazi ili
kuchukua hatua za nidhamu, lakini afanye hivyo kwa kuzingatia kwa
ukamilifu sheria, kanuni na taratibu katika Utumishi wa Umma.
Balozi
Sefue amewahimza viongozi na watumishi wa umma kuwahudumia wananchi kwa
haki, weledi, uadilifu na heshima ambapo kila ofisi ya Serikali
inapaswa kuwa na dawati la kusikiliza shida za wananchi na kuzitafutia
ufumbuzi.
Kwa
upande wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya wote nchini
wametakiwa kujenga uwezo wa kushughulikia shida za wananchi kwa
ukamilifu na kwa wakati.
“Kwa
muundo wa Serikali yetu hakuna sababu kwa mwananchi kufunga safari
mpaka Ikulu Dar es Salaam kwa kuamini kuwa ni Rais tu ndiye anayeweza
kumaliza matatizo yake, maana wawakilishi wa Rais wako kila pembe ya
nchi yetu, ikibidi wananchi wafike Ikulu inamaana hao wawakilishi wa
Rais hawakutimiza wajibu wao” aliongeza Balozi Sefue.
Aidha,
Balozi Sefue alisema kuwa ofisi zote za Serikali zinatakiwa kuwa na
dawati la kupokea maoni ya wananchi kuhusu huduma inayotolewa kwenye
ofisi hizo na kushughulikia haraka maeneo yote ambayo wananchi
wataonesha kutoridhika na huduma inayotolewa.
Post a Comment