Siku
nne baada ya majambazi 12 kuvamia Benki ya Access tawi la Mbagala,
jijini Dar es Salaam na kuiba Sh. milioni 20 na kusababisha vifo vya
watu saba, mtu anayedaiwa kuwa kinara wa uhalifu huo ametiwa mbaroni
baada ya kutajwa na washirika wake, akiwamo aliyekamatwa akiwa anafunga
ndoa.
Taarifa za uhakika zinaeleza kuwa, kinara wa ujambazi huo alikamatiwa Sinza Mori, wilaya ya Kinondoni jana, saa 11:00 jioni.
Kwa
mujibu wa taarifa hizo, kikosi kinachoshirikisha askari wa majeshi
mbalimbali ikiwamo, polisi na la wananchi wa Tanzania, kilinasa watu
wanne kwenye sherehe ya harusi baada ya kufuatilia mawasiliano yao ya
simu.
“Unajua
sasa hivi hili suala linahusisha jeshi ambao wamefuatilia kwenye
mtandao na kunasa simu za watu wanne ambao wamekamatwa huko Mbagala,
akiwamo bwana harusi na watu wengine wanne,” kilisema chanzo cha habari hii.
Taarifa
hizo zinasema baada ya watu hao kukamatwa wakiwa wanafunga ndoa
msikitini, walisaidia kutoa taarifa ambazo hatimaye zilifanikisha
kukamatwa kwa mtu huyo anayedaiwa kuwa ni kinara wa ujambazi huo.
Kamanda
wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro, alipoulizwa
kuhusu tarifa hizo alisema bado hajazipata na kwamba yawezekana
wasaidizi wake wamemkamata lakini bado hawajamfikishia taarifa.
Kinara
huyo amekamatwa ikiwa imepita siku moja baada ya Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, kutangaza uwezekano wa kutumia Jeshi la
Wananchi Tanzania (JWTZ) kushirikiana na polisi kuwasaka wahalifu wote
waliojificha kwenye misitu ya Bagamoyo na Pwani, ambako inadaiwa
walikimbilia baada ya tukio la Mbagala.
Pia
waziri huyo alisema katika operesheni hiyo, watakuwa wakiwasimamisha
mara kwa mara watumia pikipiki kwa sababu vyombo hivyo vimekuwa
vikitumiwa na majambazi katika kufanikisha matukio yao.
Post a Comment