Mkazi wa Gongo la Mboto, Omary Hamis (25) amehukumiwa kifungo cha maisha
jela baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti mtoto wa miaka tisa
ambaye ni mlemavu wa kusikia na kuongea.
Hakimu Mkazi, Flora
Haule wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, alisema mahakama imeridhishwa na
ushahidi wa mashahidi tisa ukiwamo wa daktari na fomu namba tatu ya
polisi (PF3), iliyotolewa mahakamani hapo kama kielelezo dhidi ya
mshtakiwa huyo.
“Mahakama imekukuta na hatia hivyo inakuhukumu
kifungo cha maisha jela, baada ya kupatikana na kosa la kumlawiti
mvulana wa miaka tisa ambaye ni mlemavu wa kusikia na kuzungumza, ili
iwe fundisho kwa jamii,” alisema hakimu Haule.
Katika ushahidi
uliotolewa mahakamani hapo, ilidaiwa kuwa mtoto huyo siku ya tukio
alifika kwenye banda la kuonyeshea video ambalo linamilikiwa na Hamisi
saa za jioni, kwa ajili ya kuangalia video, lakini Hamis alimfukuza
kutokana na kutokuwa na pesa ya kiingilio.
Baada ya kumfukuza
mtoto huyo aliondoka, lakini baadaye alirudi bila ya Hamis kuwa na
taarifa akakaa ndani ya banda na kisha kupitiwa na usingizi
uliosababisha abaki kwenye banda hilo peke yake hadi usiku.
Hamis alitumia mwanya huo kumlawiti mtoto huyo kwenye jumba bovu lililopo jirani na ofisi yake hiyo.
Mashahidi
waliieleza mahakama kuwa walisikia sauti ya mtu ambayo ilikuwa
haisikiki vizuri akiomba msaada, ndipo waliposogea na kumkuta Hamis
akitekeleza kitendi hicho huku akijua kuwa ni kosa kisheria.
Mashahidi
walidai hata walipomkaribia, Hamis aliendelea kutekeleza kitendo hicho
hadi walipolazimika kumpiga mateke. Hamis alikiri kuwa siku hiyo watoto
walifika kwenye banda lake hilo.
Wakili wa Serikali, Ester Kyara
aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mtuhumiwa ili iwe fundisho
kwa wote wanaotumia mabanda ya kuonyesha video kufanya ukatili kwa
watoto.
Katika utetezi wake, Hamisi alisema ana familia
inayomtegemea hivyo apunguziwe adhabu, maombi ambayo yalitupiliwa mbali
na mahakama hiyo na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.
Hamisi anadaiwa kutenda kosa hilo Agost 26, 2014 eneo la Gongo la Mboto.
Post a Comment