Mkuu
wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla ameamuru hekta 5,000 za ardhi zilizokuwa
za Chama cha Ushirika cha Luhanga Amcos zirejeshwe kwa wananchi wa
kijiji cha Luhanga wilayani Mbarali kutokana na mchakato wa kutoa ardhi
hiyo kuwa batili.
Makala
alitoa agizo hilo jana mbele ya wakazi wa kijiji cha Luhanga, katika
mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini hapo, huku akimtaka Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Mbarali, Jeremiah Mahinya
kuwachukulia hatua viongozi wa kijiji waliohusika kutoa ardhi hiyo.
“Ardhi
hiyo sasa ni ya wananchi kwa kuwa mchakato uliofanyika ni batili na
lazima Mkurugenzi uchukue hatua dhidi ya yeyote aliyehusika kwenye
mchakato huu. Iwe alighushi mihtasari au alifanya nini lazima achukuliwe
hatua”, alisema.
Alisema
wanachama wa Luhanga Amcos walikubaliana na kijiji hicho kupewa ekari
800 za ardhi kwa ajili ya shughuli za kilimo na wao kuahidi kuwa
watasaidia kutatua tatizo la maji lililokuwa likiwakabili wakazi wa
kijiji hicho ambao ni wakulima na wafugaji.
Hata
hivyo, ilielezwa kuwa baadaye nyaraka zilibadilishwa na kubainisha kuwa
ardhi waliyopewa wawekezaji hao ni hekta 5,000, hatua iliyoleta
mkanganyiko na malumbano baina ya wananchi, uongozi wa kijiji na
wawekezaji.
Alisema
pamoja na malalamiko ya ongezeko kubwa la ardhi pia wawekezaji hao
hawakutimiza ahadi ya kupeleka maji hadi sasa wakati wao wameanza
kutumia sehemu ya ardhi waliyopora kwa kijiji hicho.
Makalla
alisema, kurejeshwa kwa hekta 5,000 za ardhi kwa wananchi kunazingatia
vigezo muhimu kikiwemo cha kijiji kutoruhusiwa kuuza au kutoa ardhi
inayozidi ekari 50 kwa mtu yeyote sambamba na kutotimizwa kwa ahadi ya
kupelekwa maji kijijini hapo.
Alisema
kwa sasa serikali inahimiza kila mtu kujituma katika kazi lakini iwapo
hakuna maeneo kwa ajili ya shughuli za kilimo vijana watakuwa wanaonewa
pale inaposisitizwa kaulimbiu ya Hapa Kazi Tu.
Aliitaja
wilaya ya Mbarali kuwa miongoni mwa maeneo yanayoongoza kwa migogoro
mingi ya ardhi aliyosema mingine ni ya kujitakia au ile inayotokana na
watendaji kutosikiliza wananchi.
Post a Comment