Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, wamewakamata na kuwaondoa ombaomba 45 na 17 wamewapeleka gerezani.
Kamanda
wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro alisema jana kuwa
jeshi hilo kwa kushirikiana na Idara ya Ustawi wa Jamii, wanafanya
utaratibu wa kuhakikisha watu hao wanarudishwa mikoani walikotoka.
“Kazi
hii inaenda vizuri na ombaomba wachache wamebakia ambao wakiwaona
askari wanakimbia na kutokomea kusikojulikana,”alisema Sirro.
Katika
tukio lingine, Polisi wanawashikilia watuhumiwa 96 wenye umri wa miaka
15-18 wanaodaiwa kujihusisha na matukio ya kuvamia nyumba na kuiba
usiku.
Kamanda Sirro alisema watuhumiwa hao wanajulikana kwa jina
maarufu la ‘kumi ndani kumi nje’, walikamatwa katika maeneo mbalimbali
ya jiji na wanaendelea kuhojiwa na polisi, upelelezi utakapo kamilika
watafikishwa mahakamani.
“Watuhumiwa hawa wanavunja milango kwa mawe
makubwa na kuiba televisheni na simu, upelelezi unaendelea na
wanaendelea kutajana hivyo tutawakamata na wengine,” alidai kamanda
huyo.
Wakati huohuo, Kamanda Sirro alisema makosa ya kuvunja Sheria
ya Usalama Barabarani mkoani hapa, yameliingizia jeshi hilo mapato ya
Sh463 milioni kwa muda wa siku 10.
“Jeshi la Polisi kazi yetu ni kusimamia sheria siyo kukusanya mapato, hivyo watu wazingatie sheria,” alisema kamanda huyo.
Alisema
ili kupunguza matukio ya uhalifu, jamii haina budi kuhakikisha kunakuwa
na vikundi vya ulinzi shirikishi katika mitaa yao na Serikali za Mitaa
zinapaswa kuhakikisha jambo hilo linazingatiwa na linafanyika.
Post a Comment