Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeshauri Serikali kuharakisha ujenzi
wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge ili kuisaidia Bandari ya
Dar es salaam kukabiliana na ushindani kutoka bandari ya nchi jirani.
Hatua
hii itasaidia kuleta maendeleo ya haraka hapa nchini kupitia upokeaji
na usafirishaji wa mizigo mingi ya nchini na nje ya nchi.
Kauli
hiyo imetolewa leo mjini Dodoma na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Miundombinu Profesa Norman Sigala wakati akiwasilisha taarifa
kuhusu utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Ujenzi ,Uchukuzi na
Mawasiliano ya mwaka ujao wa fedha.
Amesema
kuwa nchi nyingine za wanachama wa Afrika Mashariki zinaendelea kujenga
reli kwa kiwango cha standard gauge kutoka Mombasa kupitia Nairobi ,
Kampala hadi Kigali kwa kasi kubwa.
Mhe.
Profesa Norman alisema kuwa ili Bandari za Tanzania ziweze kushindana
na Bandari za Kenya katika kupokea mizigo ya nchi za Uganda na Rwanda ni
vema reli ya kati ikajengwa kwa kiwango cha standard gauge ili
iziunganishe nchi hizo na reli inawezesha kusafirisha mizigo bila
vikwazo.
Aliongeza kuwa kukamilika kwa reli kwa kiwango hicho itasaidia kuwanufaisha mikoa 15 ya Tanzania bara.
Profesa
Norman alisema kuwa ni vema Serikali ikaharakisha ujenzi wa reli ya
kati na matawi yake yote ambayo ni kutoka Dar salaam kwenda kigoma,
Uvinza hadi Msongati kwa ajili ya mizigo ya Burundi.
Alisema
kuwa tawi jingine ni lile la kutoka Tabora hadi Kalemi kwa ajili ya
mizigo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC) na ile ya kutoka Tabora
kupitia Shinyanga hadi Mwanza kwa ajili ya Ukanda wa ziwa.
Kwa
upande wa Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Mhe. James Mbatia
akiwalisha maoni ya Kambi hiyo alisema kuwa reli ya kati ikiboreshwa
itasaidia kutawala soko la usafirishaji wa abiria na mizigo ya ndani na
nje ya nchi kama vile DRC, Burundi , Uganda na Rwanda.
Alisema
kuwa hivi sasa watanzania wanatakiwa kuwa na reli ambayo itaendana na
hali ya sasa inayowezesha usafirishaji wa mizigo kwa kasi na uwezo
mkubwa wa kubeba mzigo mzito.
Mhe.
Mbatia alishauri kuwa ili kufupisha ujenzi wa reli hiyo ni vema kukawa
na wakandarasi ambao watapewa vipande vidogo vidogo vya takribani
kilometa 200 ambavyo vitajengwa kwa wakati.
Naye
Waziri wa Ujenzi ,Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa
alisema kuwa Serikali kupitia Kampuni Hodhi ya Rasilimali za
Reli(RAHACO) inaendelea na uboreshaji wa miundo mbinu ya reli ili
kuongeza uwezo wa njia zilizopo za reli ya kati za kubeba mizigo mizito
zaidi.
Alisema
kuwa mara baada ya kukakamilisha uboreshaji wa reli hiyo kutasaidia
uhimilivu wa mwendo kasi wa juu na kupunguza ajali za treni.
Wizara
hiyo imeliomba Bunge kuidhinisha shilingi 4,895,279,317,500.00 kwa
ajili ya utekelezaji wa majukumu mbalimbali katika mwaka wa fedha ujao.
Kati
ya fedha hizo shilingi 2,212,141,496,500.00 ni kwa ajili ya sekta ya
ujenzi, shilingi 2,587,333,762,000.00 ni kwa ajili ya sekta ya uchukuzi
na shilingi 95, 804,059,000.00 ni kwa ajili ya sekta ya mawasiliano.
Post a Comment