
Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema kupitia mwamvuli wa Ukawa, Edward Lowassa amesema kuwa ataunda tume ya maridhiano itakayoshughulika migogoro ya wakulima na wafugaji ili kuondokana na matatizo ambayo yamekuwa yakiwasumbua.
Lowassa
amesema tume hiyo ndiyo itakayokuwa mwarobaini wa matatizo ya wakulima
na wafugaji nchini ambao wamekuwa wakipigana na kuleteana matatizo
ambayo yamechukua muda kutatuliwa.
Mgombea
huyo amesema hayo yatawezekana pale tu atakapochaguliwa kuingia
madarakani katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Akizungumza
jana na wananchi wa Matui ambao wengi wao ni wakulima na wafugaji
katika uwanja wa Soweto wilayani Kiteto Lowassa alisema tume hiyo
itapitia matatizo yote ya wakulima na wafugaji na kutoa suluhisho la
uhakika.
“Serikali
yangu itapitia migogoro hiyo na kulipa fidia zinazostahili kwa wale
walioathirika na migogoro iliyoibua mapigano kati ya wakulima na
wafugaji katika maeneo mbalimbali nchini,”alisema Lowassa huku akishangiliwa na wananchi hao.
Alisema wakishalipa fidia hizo na kutatua migogoro hiyo matatizo kati ya wakulima na wafugaji hayatajirudia tena.
Katika
Wilaya ya Kiteto kumekuwa na mgogoro wa wakulima na wafugaji ambao
umekuwa ukizungumzwa katika Bunge la 10 ukihusishwa pia na wakazi wa
Wilaya ya Kongwa.
Lowassa
alisema kuwa serikali yake itapima ardhi yote nchini ili kutambua
maeneo ya wakulima na wafugaji ili wasiweze kuingiliana na kuleteana
shida.
Kwa
upande wake aliyekuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Goodluck Ole Medeye alisema Lowassa akiingia madarakani matatizo
ya wakulima na wafugaji yatatatuliwa ndani ya miezi miwili nchini kote.
Ole
Medeye alisema kuwa Waziri Mkuu ameshindwa kutatua migogoro ya ardhi
nchini na badala yake amekuwa akitalii tu katika maeneo hayo badala ya
kusikiliza matatizo ya wananchi.
~Mpekuzi blog

Post a Comment