
Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi Dr John Magufuli akichaguliwa huenda nchi yetu ikashuhudia mapambano dhidi ya polisi na wananchi yakiongezeka kwa sababu serikali yake itaruhusu polisi kuuwa wananchi kwa kisingizio cha ujambazi.
Dr
Magufuli katika kampeni zake kwenye uwanja wa Mashujaa mkoni Mtwara 02
Septemba 2015 alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa serikali
yake haitamshitaki polisi yoyote atakayemuua jambazi mwenye silaha.
Dr
Magufuli alikaririrwa akisema ‘serikali yangu askari akipiga jambazi
mwenye silaha kwa risasi hashtakiwi. Kila mara (majambazi) wanavamia
vituo vya polisi, mbona hawavamii kambi za jeshi, jeshi la kujenga taifa
au Ukonga FFU maana polisi wana nidhamu sasa wanawaonea na kuwaua’.
Wapiga
kura wanajiuliza, kama kabla hajachaguliwa Dr Magufuli anaanza kuwaweka
wananchi roho juu kiasi hiki, je akichaguliwa mapambano kati ya
wananchi na vyombo vya dola yataongezeka kiasi gani?
Wananchi
wanauliza swali hili kwa sababu ingawa hivi sasa hakuna polisi
anayeruhusiwa kuhukumu watuhumiwa wa makosa mbali mbali ikiwa ni pamoja
na watuhumiwa wa ujambazi, lakini umma umeshuhudia polisi wakiwauwa watu
hovyo hovyo kwa tuhuma za ujambazi.
Wanauliza
je Dr Magufuli akichaguliwa na polisi wakiruhusiwa rasmi kuwauwa
watuhumiwa wa ujambazi—ni wananchi wangapi wasio na hatia watakaosukiwa
zengwe la ujambazi na kuishia kuuwawa kikatili na polisi?
Hivi
Magufuli ambaye amekuwa kiongozi wa serikali kwa zaidi ya mika 20 hajui
kwamba polisi siyo mahakama na kwamba polisi haipaswi kutoa hukumu ya
kifo kwa raia?
Wakati
mgombea Dr Magufuli akitoa ahadi kwamba kwenye serikali yake polisi
ndio watakaotoa hukumu ya kifo kwa watuhumiwa wa ujambazi; Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaelekeza kuwa ni mahakama kuu ndiyo
yenye mamlaha ya kutoa hukumu ya kifo.
Zaidi
wananchi wanajiuliza, nchi itakuwa katika hatari kubwa kiasi gani Dr
Magufuli akichaguliwa ambapo ataruhusu polisi kujichukulia sheria
mkononi kuwauwa wananchi ambao pengine maisha magumu yametumbukiza
kwenye ujambazi?
Lakini
pia wananchi wanajiuliza je Dr Magufuli uchambuzi wake wa masuala ya
kijamii umempa jibu kwamba polisi wakiwauwa ‘’majambazi wenye silaha’’
ndio utakuwa mwisho wa mapambano kati ya wananchi na polisi?
Pengine
Dr Magufuli anapaswa kujielimisha kujua kuwa chanzo cha ujambazi siyo
wananchi na wala siyo polisi. Kadhalika chanzo cha mapambano katika ya
polisi na wananchi siyo polisi wala wananchi
Dr
Magufuli anapaswa mapambano kati ya polisi na wananchi wa ni kiashiria
kimoja cha kuonyesha athari ya mfumo wa serikali ya CCM wa kutajirisha
watawala na kufukarisha wananchi wengi.
Anapaswa
kufahamu kwamba CCM baada ya kulitupa Azimiao la Arusha bila kuweka
mbadala wake katika zama hizi mpya za utandawazi wizi ambapo mfumo wa
uchumi unaotamba duniani baada ya ukomunisti kufa ni wa upebari ambao
unaruhusu mtu uwezo wa kupata apate hata kama kwa wizi na wa kukosa afie
mbali.
Matokeo
yake sasa nchi yetu Tanzania ina kikundi kidogo cha watawala
waliotajirika vya kutisha kwa kujigawia kibepari fedha za wananchi na
mali za nchi (kutumia ujambazi wa kalamu na sheria) huku mamilioni ya
wananchi wakiwepo polisi ambao hali zao za maisha ni mbaya wakitumia
mbinu mbali mbali safi na chafu ukiwepo ujambazi ili maisha yaende.
Hali
hii ni hatari kwa mustakabali wa amani ya nchi yetu. Lakini cha
kushangaza ni kwamba Dr Magufuli hajui kwamba hata pale mamilioni ya
wananchi walipotaka kuisaidia nchi kuondoa mfumo huu wa utawala
unaozalisha makundi mengi ya kihalifu katika jamii—majambazi, panya
road, wezi wa kutumia kalamu na sheria na kadhalika, CCM na serikali
yake walikataa.
Wananchi
walipendekeza Katiba Mpya CCM na serikali yake ikakataa kata kata na
kuyazika maoni hayo pale Dodoma tena kwa mbwembwe na kutukana wananchi
mwaka 2014.
Kiburi
na jeuri ya watawala wa serikali ya CCM kukataa ushauri wa wananchi
kutengeneza Katiba Mpya inayotokana na maoni ya wananchi ili kupunguza
pengo la utajiri kati ya watawala na wananchi ndiyo sababu ya wananchi
kuikataa CCM hata kama CCM itafanya propaganda na ufisadi kuonyesha
inapendwa.
Tena
wananchi wanajua kuwa Dr Magufuli akichaguliwa kuwa Rais maana yake ni
kwamba serikali ya CCM kuendelea kuwa madarakani na hivyo ujambazi
hautakwisha kwa kuuwa majambazi.
Badala
yake amani ya nchi itawekwa rehani kwa sababu kwa polisi kuua
majambazi—hasira ya wananchi itaongezeka siyo tu dhidi ya polisi bali
dhidi ya kila chombo ambacho serikali itakitumia kudhibiti umma
unaotamani madadiliko ya mfumo wa uongozi unaowafanya wananchi kuwa
maskini na kudhalilishwa na vyombo vinavyopaswa kuwalinda raia.
Kwa
hiyo vema CCM wakati huu wa kampeni isijidanganye, iwe ni kwa kutumia
tafiti za kimkakati ama propaganda nyingine zozote kuwa wanakubalika kwa
mamilioni ya wananchi wanaoteseka kwa umaskini na hivyo eti watashinda
uchaguzi.
CCM
na mgombea wao wa Urais Dr Magufuli wanapaswa kuwa na miwani
itakayowaelekeza kuona kuwa kitendo cha wananchi wenye silaha
(majambazi) kuvamia kituo cha polisi na kuuwa polisi, ni ishara tosha ya
amani kutoweka nchini –maana ni mwanzo wa vita kati ya wananchi na
polisi—kati ya wananchi na serikali yao.
Hii
ni ishara tosha kwamba wananchi wameichoka serikali ya CCM iwe
inaongozwa na Dr Magufuli au mwanamuziki maarufu nchini Diamond au mwana
CCM yeyote mwingine atakayedhaniwa ni kivutio kwa wananchi.
Kadhalika
CCM wanapaswa kufahamu kuwa kwa wananchi wengi kushabikia upinzani ni
ishara nyingine tosha kwamba wananchi wameichoka CCM na serikali yake.
Hivyo suluhisho siyo kuuwa upinzani, bali nchi kuweka mfumo mpya wa
utawala ambao misingi yake wananchi wamependekeza kwenye Rasimu ya
Katiba Mpya.
Kwa
hiyo kama kweli CCM na serikali yake wanaitakia mema Tanzania yetu
---hasa amani ya kweli unaotokana na wananchi wengi kuridhika na maisha
badala ya viongozi peke yake kuwa matajiri wa kukufuru, ni vema na ni
muhimu sana wakaheshimu maamuzi ya wananchi watakayoyafanya kupitia
sanduku huru la kura hapo tarehe 25 Oktoba mwaka huu 2015. Mungu ibariki
Tanzania.
Note:
Ninaruhusu yeyote mwenye kutaka kuisambaza, kuichapisha Makala hii
afanye hivyo. Lengo sote tushiriki kuijenga Tanzania yetu.
Ananilea Nkya
E-mail: ananilea_nkya@yahoo.com
~Mpekuzi blog

Post a Comment