
Mgomea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, ameionya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kwamba kama haitakuwa makini, inaweza kuvuruga uchaguzi mkuu.
Lowassa
ambaye anaungwa mkono na vyama vinne vya siasa vinavyounda Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa), alitoa tahadhari hiyo alipokuwa akihutubia
mkutano wa kampeni katika viwanja vya Sabasaba, mjini Magu jana.
Alitoa
kauli hiyo kutokana na takwimu za wapigakura zilizotolewa na Rais
Jakaya Kikwete juzi, zikionyesha kutofautiana na takwimu za NEC.
Akizungumza
katika kilele cha mbio za mwenge mjini Dodoma juzi, Rais Kikwete
alisema Watanzania waliojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la
Wapigakura kwa Tanzania Bara ni milioni 28 na Zanzibar ni zaidi ya 500,000.
Wakati
Rais Kikwete akitoa kauli hiyo ambayo baadaye ilisahihishwa na
mwandishi wake msaidizi, Premi Kibanga, takwimu za NEC zinaonyesha
waliojiandikisha Tanzania Bara ni milioni 22.7 na Zanzibar ni 503,193.
Lowassa
katika maelezo yake kwenye mkutano huo wa kampeni, alionyesha
kutoridhishwa na kauli ya Rais Kikwete kwa kile alichosema inatia shaka
kutokana na hali ya kisiasa ilivyo nchini.
“Jana
(juzi) Rais Kikwete alitoa kauli kuhusu idadi ya wapigakura, lakini
baadaye kauli hiyo ikabadilishwa na kukanushwa kwa sababu ilikuwa
ikitofautiana na na ile ya NEC.
“Katika
hili, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ina kazi kubwa, wasipoangalia
watavuruga, na uchaguzi ukivurugwa ni mwanzo wa matatizo katika nchi.
“Mimi
sielewi, rais wa nchi anapewaje takwimu alafu baada ya saa mbili
zinakanushwa. Huyo anayempa rais wa nchi matakwimu ya namna hiyo ni
nani? Tulisema tume ni huru je, ni huru kwa hali hii ikiwa inangojea
taarifa ambazo zinatofautiana na za rais?
“Nataka
kutoa tahadhari na kuwaomba wawe makini, wasituharibie uchaguzi,
wasituharibie nchi yetu, dhamana ya amani na utulivu juu ya mambo haya
iko juu yao, nawasihi sana wawe makini wasituharibie nchi,” alisisitiza Lowassa.
Pamoja na suala hilo, Lowassa alizidi kuzungumzia tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana nchini na kusema hilo ni sawa na bomu.
“Mtu amesoma vizuri, anakaa nyumbani, kunakucha leo, kunakucha kesho, na kila siku hivyo hivyo, haiwezekani, atafanya lolote.
“Katika
kukabiliana na hali hiyo, alisema Serikali yake itaboresha kilimo na
kukifanya kiwe cha kisasa ili kiweze kuajiri watu wengi,” alisema.
Alisema sera ya kufuta kodi zote kwenye mazao ya chakula, inalenga kuhakikisha mkulima anafaidika na kilimo.
Njia
ya pili aliyosema ataitumia kutoa ajira kwa Watanzania, ni kuhakikisha
Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) linaongezewa uwezo mara tano zaidi ya
lilivyo sasa, ili pamoja na mambo mengine, litoe zaidi mafunzo ya ufundi
na stadi zitakazowawesha vijana kujiajiri.
Mbowe atoa elimu mpya kwa wapigakura
Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe, ambaye pia ni Mwenyekiti mwenza wa Ukawa,
akizungumza na wananchi hao, alitoa elimu kwa wapigakura, aliyosema
inalenga kuokoa kura ambazo zinaweza kuharibika.
“Ukishapiga
kura yako, ukunje karatasi wakati picha za wagombea zikiwa zinaangalia
nje, tofauti na ilivyozoeleka ambapo karatasi hukunjwa picha na majina
ya wagombea yakiwa ndani. Lengo la kukunja kura picha za wagombea zikiwa
nje ni kuepuka kura za maruhani ambazo zitaharibika.
“Nawashauri
pia wote mnaoweza kubeba kalamu zenu na kwenda nazo vituoni, mwende
nazo wala msiziamini zile za NEC. Mkishapiga kura kaeni mita 200 ili
kuzilinda.
“Wanasema
tukipiga kura tukalale, hapa hakuna kulala, nyumbani hatuendi,
tutahesabu mita 200 tutapiga kambi mpaka matokeo yatangazwe, uchaguzi ni
maisha yetu na uchaguzi wa mwaka huu ni wa mabadiliko.
“Sisi
tunasema hatutaki magari yasiyohusika kuingia vituoni, mkienda kulala
wataiba kura, polisi simamieni kura, msitake kuingiza taifa kwenye
machafuko, sisi tutasubiri matokeo, tutakesha hata kama yatatoka kesho
yake,” alisema Mbowe.
Post a Comment