
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema mafisadi wamo hadi ndani ya chama chake na ndiyo maana baada ya kuteuliwa kuwa mgombea urais wengi wao wameanza kuweweseka kutokana na hofu kubwa waliyo nayo dhidi yake.
Akizungumza
kwa nyakati tofauti katika mikutano ya kampeni ya chama chake mjini
Kisarawe, Pwani na baadaye Ukonga, jijini Dar es Salaam jana, Magufuli
alikiri kuwa chama chake kiliwalea walarushwa na mafisadi kwa muda mrefu
na ndiyo maana baadhi ya watu walianza kukichukia.
Hata
hivyo, alisema tatizo hilo halitakuwapo tena kwani atakapoingia
madarakani baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, atahakikisha kuwa
mafisadi wote wanashughulikiwa bila woga.
“Ndugu
zangu, nasema kweli mafisadi hawako upinzani tu... ni ngumu sana mtu
aliye ndani ya CCM kuyasema haya, lakini lazima niseme ukweli maana
msemaukweli ni mpenzi wa Mungu. Haya mafisadi ndiyo yametufikisha hapa
na (sasa), lazima tuyashughulikie,” alisema Magufuli na kushangiliwa na wananchi waliojitokeza kwenye mkutano wake wa Ukonga.
Magufuli
aliwataja kwa sifa za jumla mafisadi waliopo kuwa ni pamoja na baadhi
ya viongozi wa serikali, ambao hujihusisha na vitendo vya rushwa na
dhuluma dhidi ya wananchi kiasi cha kuifanya serikali ichukiwe na baadhi
ya wananchi wake.
Akitolea
mfano, Magufuli alisema ni aibu kuona serikali ikikimbizana na
mamalishe na wafanyabiashara ndogondogo (Wamachinga) ili kupata kodi
wakati kuna baadhi ya nchi ambazo zinaendeshwa kwa mapato ya bandari tu.
Magufuli
aliongeza kuwa anatambua wananchi wamekuwa wakinyanyaswa katika maeneo
mbalimbali ikiwamo kutozwa kodi zisizosaidia kuinua pato la taifa bali
kuwafaidisha baadhi ya viongozi na kwamba, kwa sababu hiyo, haoni sababu
ya kuendelea kwa hali hiyo hasa kwa kujua kuwa kuna nchi zinajiendesha
kwa mapato ya bandari.
Alisema
yote hayo ni baadhi ya mambo anayoamini kuwa ni sababu ya yeye
kuchaguliwa kuwa rais ili kudhibiti uonevu kwa wanyonge na pia kupambana
na mafisadi serikalini, ambao wamezoea kuishi kwa rushwa na ulaghai.
Kwa
mfano, alisema anajua namna ambavyo baadhi ya watumishi bandarini
huruhusu makontena kupita bila kulipiwa ushuru na kuikosesha serikali
mapato yake ili kuwahudumia wananchi.
“Wapo
watu wanaikosesha serikali mapato. Hawa nataka nikapambane nao... na
nitapambana nao kweli kweli. Na hawatanikwepa…najua wananiogopa na
wameanza kumwaga hela ili nishindwe. Nyinyi hela zao kuleni maana ni
kodi zenu, lakini kura ni kwa Magufuli,” alisema.
Barabara za juu Tazara
Katika
hatua nyingine, mgombea huyo alisema ujenzi wa barabara za juu kwenye
makutano ya Tazara, Dar es Salaam utaanza muda wowote kwani mkandarasi
ameshapatikana.
Dk.
Magufuli alisema kuwa serikali ya Tanzania imeshatiliana saini na
serikali ya Japan kwa ajili ya ujenzi huo kwani hata michoro
imeshakamilika.
Alisema
katika makutano ya Ubungo, kutajengwa barabara ya juu ya ghorofa tatu
ili kuwezesha magari mengine kupita juu, mengine katikati na mengine
chini ili kupunguza msongamano.
Aahidi Kuwasainisha Mikataba Mawaziri Wake
Kuhusiana
na uteuzi wa baraza lake la mawaziri, Magufuli alisema atateua mawaziri
wachapakazi na si wale wa kukaa ofisini huku shughuli nyingi za
maendeleo zikikwama.
Alisema
anataka mawaziri atakaowateua kuiga mfano wake kwa kushinda kwenye
miradi ya maendeleo ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati.
Dk.
Magufuli alisema kama yeye angekuwa mtu wa kushinda ofisini na kutoa
maagizo, huenda barabara za lami zinazofikia kilomita 17,000
zisingekuwapo kwani makandarasi wengi walionyesha uzembe aliwafukuza.
“Kama
mimi nilianguka kwenye helikopta (chopa) nikikagua mafuriko Dar es
Salaam, nikalala daraja la Dumila Morogoro, nao wafanye hivyo…kama ni
Waziri wa Maji, basi ashinde kwenye miradi ya maji, kama ni barabara
basi ashinde barabarani kuhakikisha zinajengwa kwa kiwango,” alisema na kuongeza.
“Nikishinda
na kuingia Ikulu nitakuwa nawahoji mawaziri nitakaowateua kama watamudu
majukumu yao ama la na yule atakayekubali kwamba anaweza basi atasaini
na akishaini ole wake nimpe kazi halafu ashindwe kumudu majukumu yake.”
Awapiga kijembe wanaofagia barabara
Katika
hatua nyingine, Dk. Magufuli aliwashangaa wanaopiga deki barabara za
lami ili wagombea wao wapite huku wakibeza kwamba serikali ya CCM
haijafanya lolote.
Aliwataka
waendeleze utaratibu wa kupiga deki barabara ili ziwe safi hata baada
ya uchaguzi ili kuwaonyesha ni namna gani serikali ya CCM imejenga
barabara nyingi za lami.
“Huwezi
kupiga deki barabara ya vumbi, huwezi kupiga deki barabara yenye
mashimo, wanatusema wakati wanapita kwenye barabara hizo hizo za lami
tulizojenga,” alisema Magufuli.
Hivi
karibuni, baadhi ya wananchi wa mji wa Musoma mkoani Mara na Mkoani
Mwanza walijitokeza kupiga deki barabara kabla ya kutumiwa na mgombea
urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anayeungwa mkono na
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa. Mbali na Chadema,
Ukawa inaundwa na CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.
Post a Comment