MVUA kubwa imenyesha mkoani Mwanza na kusababisha maafa, ikiwemo vifo vya watu wawili na familia kadhaa kukosa makazi kutokana na nyumba kubomoka.
Aidha, mvua hiyo imesababisha kufungwa kwa muda uwanja wa ndege wa Mwanza kutokana na kujaa maji.
Mvua hiyo
inasadikiwa ndiyo mwanzo wa El-Nino kutokana na taarifa ya Mamlaka ya
Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kueleza jana kwamba, kutakuwa na mvua za
El-Nino, kama ilivyokuwa imeelezwa katika taarifa yake ya Septemba mwaka
huu.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo katika mkutano wake na
waandishi wa habari, alisema mmoja wa waliopoteza maisha, ni mwendesha
bodaboda wa Kirumba aliyekuwa amepakiza wanafunzi wawili akiwapeleka
shuleni.
Kuhusu
wanafunzi hao, Kamanda alisema, taarifa zake hazijathibitishwa kama pia
wao wamepoteza maisha, ingawa tukio hilo limo katika orodha ya athari
za mvua hizo.
Alisema mtu mwingine alionekana akiwa anaelea katika maji eneo la Mabatini, lakini baadaye mwili wake haukuonekana kutokana na mafuriko hayo.
Alisema mtu mwingine alionekana akiwa anaelea katika maji eneo la Mabatini, lakini baadaye mwili wake haukuonekana kutokana na mafuriko hayo.
“Tumepokea
taarifa juu ya mvua hizi kutoka maeneo mbalimbali ya jiji la Mwanza na
tunaendelea kukusanya taarifa na kuchukua hatua stahiki,” alisema Kamanda Mkumbo.
Kuhusu
uwanja wa ndege, mvua hizo zilisababisha kufungwa kwa saa tano kwa
uwanja wa ndege wa Mwanza baada ya kujaa maji. Meneja wa uwanja wa Ndege
wa Mwanza, Esther Madale alimwambia mwandishi wa habari kwamba uwanja
huo ulilazimika kufungwa kwa saa tano kwa ajili ya kuwezesha wahandisi,
kufanya uchunguzi wa miundombinu yake.
Hakuna ndege iliyoruhusiwa kutua katika muda huo.
“Ni kweli tulikumbwa na mkasa huo wa mvua ambazo zilinyesha mfululizo
na kusababisha kufungwa kwa uwanja kwa muda…kwa sasa tunavyoongea tayari
huduma zimerejea katika hali yake ya kawaida,” alisema Madale.
Uwanja
huo wa ndege upo katika matengenezo makubwa, ikiwamo mnara wa kuongozea
ndege, njia za kurukia ndege ambazo sasa ni meta 2000 na zinaongezwa
hadi kufikia meta 3300. Ukarabati huo ulianza mwaka 2012 na ulitarajiwa
kumalizika Oktoba mwaka huu.
El-Nino imeanza
Katika
taarifa ya TMA kwa vyombo vya habari jana, ilisema kuendelea kuongezeka
kwa joto katika maeneo ya Bahari ya Pasifiki kunaonesha kuimarika kwa
mvua za El-Nino kama ilivyoelezwa katika taarifa iliyotolewa Septemba,
mwaka huu.
Taarifa
hiyo iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, imesema mvua
zimeshaanza kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini hususani Ukanda wa
Ziwa Viktoria, Kanda ya Magharibi na Nyanda za Juu, Kaskazini Mashariki
na zinataraji kuwa za juu ya wastani.
“Hata
hivyo, mifumo mingine ya hali ya hewa ikiwemo mwitikio wa mfumo ya hali
ya hewa katika Bahari ya Hindi imekuwa na mchango hasi kinyume na
ilivyotarajiwa katika mwenendo wa mvua za Vuli nchini katika kipindi cha
mwezi Oktoba, 2015 na kusababisha vipindi virefu vya upungufu wa mvua
katika mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es Salaam,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha
taarifa hiyo ya Dk Chang’a ilisema maeneo yanayopata mvua mara moja kwa
mwaka mikoa ya Dodoma, Singinda, Ruvuma, Lindi, Mtwara, Songea, Mbeya,
Iringa, Njombe, Tabora, Kigoma Rukwa na Katavi mvua zinatarajiwa kuanza
kati ya wiki ya pili na ya nne ya Novemba, 2015.
Alisema
mvua hizo zimeanza kujiimarisha katika mikoa ya Kigoma, Tabora na
Katavi na zinatarajiwa kusambaa katika maeneo mengine mwezi huu. Hata
hivyo, wilaya za Kondoa, Kongwa na Singida Vijijini katika mikoa ya
Dodoma na Singida, zinatarajiwa pia kupata vipindi vya mvua mwanzoni mwa
mwezi huu.
Mamlaka
hiyo imeshauri wananchi, hususani wafugaji, Mamlaka za Wanyamapori,
Mamlaka za Maji na Afya waendelee kutafuta, kupata na kufuata ushauri wa
wataalamu katika sekta husika katika kutekeleza mipango inayoweza
kuathiriwa na mwelekeo wa hali ya hewa iliyotabiriwa. Aidha mamlaka
imetaka wananchi na wadau kwa ujumla kuzingatia hadhari mbalimbali
zilizokwisha kutolewa.
Taarifa
hiyo imesema mwelekeo wa mvua uliotolewa umezingatia zaidi viashiria
vya mvua katika kipindi cha msimu (miezi mitatu) na hali ya mvua katika
maeneo makubwa.
Hivyo,
viashiria vinavyochangia mwenendo wa mifumo ya mvua na mabadiliko ya
muda mfupi katika maeneo madogo utazingatiwa katika uchambuzi wa utabiri
wa muda wa kati na mfupi.
TMA imeahidi kuendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa taarifa za mwelekeo wa mvua nchini.
Post a Comment