POLISI Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imepiga marufuku maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), yaliyopangwa kufanyika bila ukomo kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni kinyume cha sheria.
Kamanda
wa Kanda hiyo, Suleiman Kova aliwaambia waandishi wa habari jana
ofisini kwake, jijini Dar es Salaam, kwamba maandamano hayo yana
viashiria vya uvunjifu wa amani.
Maandamano
hayo yaliyotajwa kuwa hayana kikomo, yalipangwa kufanyika katika maeneo
yote ya jiji la Dar es Salaam. Kova alisema kama yakiruhusiwa, yatakuwa
chanzo cha mfarakano mkubwa nchini, jambo ambalo litaathiri amani na
maisha ya Watanzania.
Alisema
maandamano hayo ni jambo ambalo haliwezekani, kwani pia yatasababisha
msongamano mkubwa kwa wakazi wa jiji hilo na watapata usumbufu kwa
kushindwa kufanya shughuli zao kwa ufasaha.
Alisema
walipokea barua yenye Kumbukumbu namba CDM/PW/ GEN/042/2015
iliyoandikwa Oktoba 31, lakini iliwasilishwa ofisini kwake jana, ikitoa
taarifa ya kufanya maandamano leo.
“Katika
barua hiyo, Chadema Kanda ya Pwani walitoa taarifa ya kufanya
maandamano ya amani yasiyo na kikomo kuanzia kesho (leo) katika maeneo
yote ya jiji la Dar es Salaam kupinga kile walichodai ni uporwaji wa
demokrasia dhidi ya mgombea wao wa urais Edward Lowassa ambaye wamedai
ndiye mshindi,” alisema Kova.
Alisema
baada ya kusoma barua hiyo kwa makini na kutafakari, amebaini kuwa
kutokana na Sheria ya Polisi na Polisi Wasaidizi Sura ya 322 Kifungu cha
43 (1) kama ilivyorekebishwa mwaka 2002, taarifa ya maandamano
inatakaiwa itolewe saa 48 kabla ya muda wa kuanza maandamano, kitu
ambacho kimekiukwa, kwani barua hiyo ilipelekwa ofisini kwake jana.
“Kwa
mujibu wa sheria hii, Chadema hawataruhusiwa kufanya maandamano hayo
kutokana na kuchelewa kutoa taarifa kwa wakati. Wamemtaja Lowassa kuwa
ndiyo mshindi, lakini kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya
Mwaka 1977, Tume ya Taifa ya Uchaguzi ndiyo ina mamlaka ya kumtangaza
mshindi,” alisema.
Alisema
maandamano hayo ni batili na ni kinyume cha Sheria. Alisema kama
hawakuridhika na uamuzi huo wa polisi, wanaruhusiwa kukata rufaa kwa
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi chini ya Kifungu Namba 43 (6) ya Sheria
za Polisi na Polisi Wasaidizi Sura ya 322.
Hata
hivyo, Kova alisema barua hiyo iliyowasilishwa na Chadema imeandikwa
huku ikitawaliwa na shari; na pia inaonekana taarifa hiyo lengo lake ni
kuvuruga amani.
“Nawaomba
viongozi wa Chadema watumie busara, wasitake kuiingiza hii nchi katika
matatizo na umwagaji damu, Watanzania sisi ni watu wa amani, hatujazoea
haya mambo. Kuna taratibu na sheria wazifuate hizo,” alisema.
Alisema
polisi wamejipanga vizuri kuhakikisha nchi inakuwa salama na
atakayekaidi agizo hilo, atachukuliwa hatua kali za kisheria. Pia,
alitaka vijana wasikubali kutumiwa katika kuvuruga amani.
Post a Comment