
Bei
ya umeme inatarajia kushuka wakati wowote kuanzia sasa baada ya Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (pichani )kuliagiza
Shirika la Umeme (Tanesco), kushusha gharama za nishati hiyo.
Katika
hatua nyingine, Waziri huyo amefuta likizo za wafanyakazi wa shirika
hilo ili washughulikie tatizo la umeme nchini huku akisisitiza kuwa
hataki kusikia kukatika katika kwa umeme.
Profesa
Muhongo alitoa maagizo hayo jana jijini Dar es Salaam wakati
alipofanya ziara ya kushtukiza katika mtambo wa kuzalisha umeme wa
Tegeta Gas Plant, ambapo alikwenda kwa ajili ya kukagua mitambo hiyo ili
kuona kama yote inafanyakazi.
Akitoa maelezo ya mtambo huo, Meneja Mohamed Kisiwa alisema wana mitambo mitano na wana uwezo wa kuzalisha Megawati 42 kila saa.
Alisema gharama ya uzalishaji umeme kwa uniti moja ni Sh. 90 na wamekuwa wakiuza kwa Sh. 180 hadi 187.
Profesa
Muhungo alisema kwa maelezo ya meneja huyo, inaonyesha umeme
wanaozalisha wanapata faida mara mbili hivyo alisema kuna uwezekano
mkubwa wa kushusha gharama za umeme.
Aliagiza maofisa wa wizara yake na wa shirika la Tanesco wakutane leo ili wajue umeme huo utashushwa kwa kiwango gani.
“Utauzaje
umeme mara mbili ya gharama za uzalishaji, tunataka kuwapunguzia
wananchi bei ya umeme na kwenye mkutano wetu wa kesho (leo) tutajadili
kupunguza bei ya umeme..haya mahesabu hayajakaa sawa maana unazalisha
uniti moja kwa Sh. 90 na kuuza kwa Sh. 180 tutajadiliana mpunguze,”
alisema.


Post a Comment