Sekretarieti
ya Maadili ya Viongozi wa Umma imemkabidhi Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
majina ya baadhi ya mawaziri na naibu mawaziri ambao hawajajaza fomu za
mali wanazozimiliki kama sheria inavyowataka.
Akizungumza
jana kwenye semina ya mawaziri na naibu mawaziri, Kamishina wa
Sekretarieti hiyo, Jaji mstaafu Salome Kaganda alisema viongozi hao
wanajua umuhimu wake lakini wanapuuza.
“Sheria
hii ya Maadili ya Viongozi wa Umma inajulikana, lakini jambo la
kushangaza wapo baadhi ya mawaziri na manaibu ambao hawajajaza, kwa
ruhusa yako nitakukabidhi majina yao, sisi tunafanya kazi kwa mujibu wa
sheria, hivyo anayekiuka anapaswa kuadhibiwa,” alisema Jaji Kaganda bila kutaja majina hayo.
Kifungu
cha 9 cha sheria hiyo kinataka katika kipindi cha siku 30 baada ya
kupewa wadhifa, kila mwisho wa mwaka na mwisho wa kutumikia wadhifa wake
kiongozi husika anatakiwa kupeleka tamko la maandishi la mali zake.
Sheria
hiyo inafafanua kuwa mali hizo ni pamoja na rasilimali zake au mume au
watoto wenye umri usiozidi miaka 18 ambao hawajaoa au kuolewa.
Alisema
fomu hizo lazima zijazwe na viongozi na wananchi wanaruhusiwa kwenda
kuzihakiki wakitoa sababu za msingi, lakini sheria hiyo hairuhusu waende
kutangaza na wakifanya hivyo hatua zinachukuliwa dhidi yao.
“Hapo ndipo wananchi wengi huwa hawatuelewi kwa kuwa wanapenda kujua mali ambazo viongozi wao wanamiliki,” alisema.
Alisema
Sekretarieti kwa kutambua umuhimu wa viongozi hao kuzingatia sheria na
maadili, ndiyo sababu imeandaa semina hiyo baada ya kupata ufadhili
kutoka Shirika la Misaada ya Maendeleo la Marekani (USAID), wakiamini
kuwa yatasaidia kuwakumbusha.
Post a Comment