SERIKALI imesema bajeti ya mwaka ujao, hususani utekelezaji wa miradi yote ya maendeleo, itatekelezwa kwa fedha za ndani.
Waziri
wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema miradi mikubwa kama vile
ujenzi wa reli ya kisasa ya kati na miradi mingine mikubwa, ndiyo
itajengwa kwa fedha za msaada kutoka nje kwa kuwa nchi haiwezi kukwepa
kuomba msaada kutoka nje.
Alisema
hayo jana katika mji mdogo wa Holili mpakani mwa Tanzania na Kenya,
baada ya kuangalia shughuli za utendaji kazi katika mpaka huo na baadaye
kuzungumza na wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato (TRA) katika mji huo.
Alisema
makusanyo ya sasa ya Sh trilioni 1.7 kwa mwezi yanayokusanywa kwa sasa
nchi nzima, fedha zake zitaelekezwa kwa shughuli za maendeleo kwa mikoa
yote nchini.
Waziri huyo alisema si kweli kwamba serikali ya Rais John Magufuli haitahitaji msaada wa fedha kutoka nje. “…la hasha! ila msaada huo hautakuwa mkubwa kama zamani,” alisema waziri.
Akizungumzia bajeti ijayo, alisema fedha zake nyingi zitatokana na makusanyo ya fedha za ndani na sio za msaada kutoka nje.
Waziri
huyo alisema kwa asilimia kubwa bajeti ya miradi ya maendeleo katika
mikoa yote nchini, fedha zake zitakuwa ni za ndani zilizokusanywa na
kiasi kidogo cha fedha kitatoka nje.
Aliwataka
watumishi wote wa umma, wanaokusanya mapato katika maduhuli ya
serikali, kuacha mara moja kushika na kukusanya fedha kizamani kwa
kutumia stakabadhi na kuandika kwa mkono ili kuepuka ushawishi wa
kutumia fedha hizo kwa njia isiyokuwa halali.
Alisema
anasikitishwa na utaratibu wa ofisa uhamiaji wa kitengo viza cha mji wa
Holili, kukaa na fedha zaidi ya siku tano na kutoa stakabadhi kwa
mkono.
Waziri
alikemea na kumtaka ofisa wa uhamiaji wa mji wa Holili, kuacha mara
moja kukaa na fedha za serikali kwa zaidi ya wiki, tofauti na mtunza
fedha wa TRA anayepeleka fedha benki kila siku.
Alisema
utaratibu huo ulishapigwa marufuku miaka mitatu iliyopita, lakini
anasikitika unaendelea katika mji wa Holili. Alimwagiza Mkuu wa Uhamiaji
Mkoa wa Kilimanjaro, kubadilisha hali hiyo kwa maslahi ya serikali.
Akizungumzia
uadilifu, Waziri Mpango aliwataka wafanyakazi wa TRA, kuacha kufanya
kazi hiyo kwa kuwanyanyasa wafanyabiashara, kwani kufanya hivyo ni kosa
kisheria. Alisema uadilifu si wa mali tu, bali uko pia katika kutenda
kazi za kila siku.
Alisema
pia wananchi wanapaswa kulipa kodi kwa kufurahia na kuona kodi
wanayolipa inawanufaisha, ikiwa ni pamoja na kufanya maendeleo katika
miradi mbalimbali.
Post a Comment