Mwanasiasa
mkongwe nchini, Steven Wasira jana alimvamia mpigapicha wa gazeti la
Mwananchi aliyekuwa akichukua picha zake wakati akitoka mahakamani,
lakini akashindwa kutimiza azima yake ya kufuta picha.
Wasira,
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika wa Serikali ya Awamu ya Nne
(SA4), alifanya kitendo hicho akitoka kwenye jengo la Mahakama ya
Biashara ambako maombi yake ya kukata rufaa ya kupinga matokeo ya
uchaguzi wa ubunge, jimbo la Bunda yalitupwa na Mahakama Kuu.
Katika
kinyang’anyiro hicho cha ubunge, Wasira, ambaye amekuwa mbunge wa
Mwibara tangu mwaka 1970 na baadaye mbunge wa Bunda hadi mwaka 2015,
aliangushwa na Ester Bulaya wa Chadema katika uchaguzi wa Oktoba 25
mwaka jana. Waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari akiwamo
walishuhudia tukio hilo.
“Wasira alimkimbiza Jamson akitaka kumnyang’anya kamera, lakini hakuweza,” alisema Nyange,mwandishi wa gazeti la Mtanzania.
“Baadaye alitaka kumgonga kwa gari lake wakati akiondoka lakini ikashindikana.”
Akisimulia
tukio hilo, Jamson alisema Wasira, ambaye amefanya kazi na serikali za
awamu zote tangu katikati ya miaka ya 70, alichukizwa na kitendo chake
cha kumpiga picha.
“Wasira alinifuata na kuniuliza sababu za kumfuatilia kila mara. Aliniuliza picha nazopiga nazipeleka wapi,” alisema Jamson.
“Njoo,
njoo hapa wewe kijana. Nakuambia futa hizo picha kwa usalama wako.Hivi
mnatafuta nini maana mnanifuatilia tangu nikiwa kule Mahakama Kuu hadi
huku Mahakama ya biashara,” alisema Wasira
Jitihada
za Wasira kumnasa Jamson ziliendelea hadi nje ya eneo la mahakama
ambako alimfuata kwa kutumia gari aina ya Toyota Land Cruiser (namba
tunazihifadhi).
Katika
kumfuatilia, gari la Wasira nusura limgonge mpigapicha huyo, lakini
waandishi wenzake walimnusuru kwa kumsukumia pembezoni mwa barabara.
Juhudi
za kumpata Wasira kuzungumzia sababu za kutaka kumshambulia mpiga picha
huyo kwa kuchukua picha za tukio hilo, hazikuzaa matunda.
Awali,
Jaji Sirilius Matupa alitupilia mbali maombi ya ruhusa ya kukata rufaa
dhidi ya uamuzi wa kufuta shauri la kupinga matokeo ya uchaguzi wa Bunda
baada ya kubaini waliowasilisha maombi hayo, Magambo Masato na wenzake
wanne, hawakufuata sheria.
Uamuzi huo ulisomwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Eugenia Rujwahuka kwa niaba ya Jaji Matupa.
Katika
maombi yao ya msingi, Magambo Masato na wenzake waliiomba mahakama
kutengua matokeo yaliyompa ushindi Bulaya wakidai licha ya Wasira
kunyimwa haki kuhakiki na kuhesabu upya kura, mchakato wa uchaguzi huo
pia uligubikwa na vitendo vya rushwa.
Akisoma
maamuzi hayo kwa niaba ya Jaji Sirilius Matupa, Naibu Msajili wa
Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Eugenia Rujwahuka alisema maombi hayo
yamewasilishwa kwa kutumia kifungu cha sheria kisichohusika.
“Badala
ya kuwasilisha maombi yao kwa kutumia kifungu cha 15 (c) cha Sheria ya
Uchaguzi Sura namba 141, waleta maombi wametumia kifungu cha 15 (a)
(b),” alisema Rujwahuka akimnukuu Jaji Matupa.
Wakati
huohuo, shauri la kupinga matokeo ya uchaguzi wa jimbo la Nyamagana,
iliyofunguliwa Ezekiah Wenje, imesikilizwa jana na kuahirishwa hadi
Februari 29, mwaka huu.
Akiahirisha
shauri hiyo iliyoahirishwa mara mbili mfululizo Jumatatu na Jumanne
iliyopita, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, Kakusulo
Sambo aliziagiza pande zinazohusika kuhakikisha zinakamilisha taratibu
zote za kisheria ili shauri hilo lianze kusikilizwa mfululizo.
Post a Comment