Ikulu
imeahidi kufanyia kazi madai ya Chama cha Wasanii Wachoraji Tanzania
(Chawata), ambayo waliyawasilisha jana, kikilalamikia ofisi hiyo katika
awamu ya nne iliyokuwa chini ya Rais Jakaya Kikwete, kuwacheleweshea
malipo yao ya Sh. milioni 53.6.
Kwa
mujibu wa taarifa ya Chawata kwa vyombo vya habari jana, fedha hizo
zimetokana na kazi za sanaa ambazo zilichukuliwa na serikali ya awamu ya
nne kutoka kwa wafanyabiashara wa eneo la Mwenge jijini Dar es Salaam
na kupelekwa Ikulu.
Hata
hivyo, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa,
alithibitisha kuwapo na madai hayo na kusema kuwa yatafanyiwa kazi ndani
ya wiki moja kuanzia jana.
“Ni
kweli Ikulu inadaiwa, lakini ni deni la awamu ya nne, kwa hiyo
tumewaomba kuwakamilishia madai yao ndani ya wiki moja, baada ya kufanya
uhakiki ili kujiridhisha,” alisema Msigwa.
Awali,
Katibu wa Chawata, Cuthbert Semgoja alisema waliahidiwa kulipwa fedha
hizo kabla ya uchaguzi mkuu mwaka jana lakini hadi sasa hawajalipwa.
"Tuliuza
kazi zetu Ikulu kwa makubaliano ya kulipwa baadaye tangu Agosti mwaka
jana, hadi leo hii (jana) bado hatujaweza kupatiwa pesa zetu," alisema na kuongeza:
“Mchakato
wa kazi zetu ulianza mwishoni mwa mwezi wa nane kwa kamati husika,
kupitia katika maeneo ya wasanii, ili kuweza kufanya chaguzi ya sanaa
wanazohitaji. Walijiridhisha kwa kuchukua baadhi ya sanaa kutoka kwa
wanakikundi kwa ahadi ya kufanya malipo mara moja kabla ya uchaguzi mkuu
lakini hadi sasa bado malipo hayo,” alisema Semgoja.
Alisema
baada ya chama kuona muda wa malipo unakwisha, walichukua jukumu la
kupiga simu kwa mhusika ambaye walikuwa wakifanya naye biashara hiyo kwa
niaba ya Ikulu, lakini jibu lake lilikuwa `malipo yenu yanaandaliwa.'
“Baada
ya mwezi mmoja kufanya biashara hiyo, tulianza kumpigia simu mtu mmoja
ambaye ndiye alikuwa anahusika na sisi tangu mwanzo wa biashara yetu
hadi mwisho, lakini majibu tunayopewa ni kusubiri tu, tumechoka sasa,” alisema.
Alisema
mawasiliano waliyokuwa wanafanya na mtu kutoka Ikulu ambaye
alijitambulisha (jina tunalo), ndiye aliyekuwa akiwapa majibu hayo
kuhusu madai yao.
Aliongeza
kuwa kulingana na ahadi waliyopewa kulipwa kabla ya uchaguzi mkuu na
mlolongo wa ahadi zinazojirudia, walianza kufanya mawasiliano wao kwa
wao ili kufahamu nini kinachoendelea kuhusu malipo yao na kugundua kuwa
kuna tatizo.
“Ilifika
hatua simu zetu hazipokelewi, kila tunapopiga mhusika hapokei simu
zetu, ndipo hapo tulipohisi kuna mchezo unaendelea kati ya mtu huyo na
chama chetu,” alisema.
Post a Comment