SERIKALI
imesema imedhamiria kurejesha heshima ya wazee wote hapa nchini kwa
kuisimamia jamii kuwathamini wazee na kuwapa kipaumbele katika huduma
zote za jamii.
Tamko
hilo limetolewa na Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Ummy Mwalimu mjini Morogoro wakati wa uzinduzi wa kampeni ya
Mzee Kwanza inayolenga kuwapa kipaumbele wazee katika huduma zote za
kijamii.
“Nataka
heshima ya wazee irudi...wapate huduma kwa kupewa heshima yao, ifike
mahali mzee anapofika sehemu yoyote akihitaji huduma apewe kipaumbele,
ni lazima tuwape heshima yao kwa sababu wameifanyia nchi mambo makubwa
wakati wa ujana wao,” alisema Waziri.
Alisema
kuwa wazee katika jamii yoyote wana nafasi kubwa katika ujenzi wa taifa
kwa kuwa wao ni hazina ya busara, hekima, amani na utulivu wa jamii
yoyote.
“Familia
isiyoheshimu wazee aghalabu itakuwa na vurugu na ugomvi kila kukicha.
Lakini jamii au familia inayoenzi wazee na kuwapa nafasi zao katika
kushauri, kukosoa na kuelekeza utendaji wa siku hadi siku, jamii au
familia hiyo itakuwa na baraka siku zote hivyo nikiwa Waziri mwenye
dhamana nitahakikisha hili linawezekana,” alisema Waziri Ummy.
Alisema
kuwa Serikali imeona ni vyema kurejea kwenye desturi hii kwa kuanzisha
kampeni maalumu ya Mzee Kwanza ambaypo ni wajibu wa kila Mtanzania kuona
kuwa anafanya kila awezalo kurejesha hadhi ya wazee na kuwapa umuhimu
wa kwanza katika kupata huduma za kijamii.
Waziri
Ummy alisema kuwa takwimu za sensa za mwaka 2012 zinaonesha kuna jumla
ya wazee 2,507,568 wenye miaka kati ya 60 na kuendelea huku kukiwa na
wazee takriban 474,053 wenye miaka 80 na kuendelea.
Alisema
kuwa ili kuhakikisha wazee wanakuwa kwenye mazingira mazuri, Serikali
kupitia Wizara ya Afya imeandaa Muswaada wa kutungwa kwa Sheria ya Wazee
ambayo itapelekwa Bungeni ili ipitishwe kuwa Sheria ambayo itasimamia
upatikanaji wa haki na ustawi wa wazee Sheria hii itatoa ahueni kubwa
kwa wazee na kuboresha sana maisha yao ya uzeeni.
Aidha
alisema kuwa Serikali imeagiza kila halmashauri kubaini wazee walio
katika maeneo yao na kuhakikisha wanapata huduma zote za msingi ikiwa ni
pamoja na huduma za afya kutoka kwenye mapato yao wenyewe.
Akizungumzia
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya aliupongeza kwa mwitikio waliochukua
kushirikiana na Wizara katika Uzinduzi wa kampeni ya Mzee Kwanza katika
huduma kwa nchi yetu.
“Najua
hamasa hii wameipata kutokana na ukweli kwamba Mfuko huu unawahudumia
wanachama wastaafu ambao nao wako katika kundi hili la wazee,
nawapongeza NHIF kwa hatua mliyochukua ya kufanya mkutano na wanachama
wenu wastaafu wiki chache zilizopita,” alisema.
Post a Comment