Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imetangaza rasmi kuingilia
kati na kutafutia ufumbuzi tatizo la rushwa katika migogoro kati ya
wakulima na wafugaji nchini.
Taasisi
hiyo imewaonya viongozi wa vijiji wenye tamaa na kuchangia kuibuka kwa
migogoro hiyo na kuwataka wakae chonjo kwani wakati wa kuishughulikia
migogoro hiyo umefika.
Hayo
yalisemwa na Mkuu wa taasisi hiyo mkoani Morogoro, Emmanuel Kiyabo
alipozungumza na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa ya kazi za
Takukuru mkoani humo kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu.
Aliwataka
viongozi wa vijiji kuachana na tamaa ya kupokea fedha kutoka kwa
wafugaji na kuingiza mifugo hovyo, hali inayosababisha uhaba wa ardhi na
migogoro baina ya wakulima na wafugaji.
Mkoa
wa Morogoro ni moja wa mikoa yenye migogoro ya muda mrefu kati ya
wakulima na wafugaji hasa wilaya za Kilosa na Mvomero ambayo wakati
mwingine imesababisha vifo vya watu na maelfu ya mifugo.
Mkuu wa Takukuru aliwataka pia wakulima kuacha tamaa ya kupokea malipo ya fidia ya mazao yao kutoka kwa wafugaji isivyo halali.
Alisisitiza
wafugaji kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za kusafirisha mifugo na
kuingiza katika maeneo mapya bila kuathiri maisha ya wenyeji wao.
Alisema
katika kipindi hicho cha miezi mitatu, taasisi hiyo ilifanya udhibiti
na kushauri idara mbalimbali za Serikali namna ya kuziba mianya ya
rushwa ikiwamo kuweka mikakati inayopimika ya kudhibiti mianya hiyo
iliyobainika.
Aidha,
alisema katika kipindi hicho pia jumla ya miradi ya maendeleo 16 yenye
thamani ya Sh bilioni 3.4 ilikaguliwa na baadhi ya miradi hiyo
iligundulika kuwa na vitendo vya udanganyifu katika matumizi ya fedha za
Serikali na kusisitiza kuwa uchunguzi unaendelea.
Hata
hivyo, alisema katika uchunguzi wanaoendelea nao wameweza kuokoa fedha
za Serikali Sh milioni 14.4 zilizokuwa mikononi mwa baadhi ya
watuhumiwa. Alisema fedha hizo zimeingizwa kwenye akaunti maalumu ya
Serikali ya fedha zilizookolewa.
Alisema
Takukuru iliokoa Sh milioni 13.2 ikiwa ni gharama ya kuweka alama za
barabarani katika Manispaa ya Morogoro, akieleza kuwa mkandarasi
alilipwa bila kuweka alama hizo katika barabara za Kitope, Kingo,
Mlapakolo na Nguzo.
Lakini
mara baada ya taasisi hiyo kuanza uchunguzi na wahusika kufahamu kuwa
wanachunguzwa, waliweka alama hizo kwa mujibu wa mkataba.
Pia
alisema katika kipindi cha kuanzia Januari mpaka Machi mwaka huu,
Takukuru ilifungua kesi 12 katika Mahakama za Wilaya za Ulanga,
Morogoro, Kilosa na Mahakama ya Mkoa ambazo watuhumiwa wake walihusika
kuomba na kupokea rushwa.
Mkuu
huyo wa Takukuru alisema katika kipindi hicho, pia taasisi hiyo mkoani
Morogoro ilipokea jumla ya taarifa 105 zinazohusisha malalamiko dhidi ya
idara na taasisi mbalimbali za Serikali ambazo ni serikali za vijiji,
mitaa, vitongoji, afya, utumishi, sekta binafsi, mabaraza ya usuluhishi,
ardhi, maliasili, kilimo, maji, jeshi la wananchi wa Tanzania,
manunuzi, mamlaka ya vitambulisho vya Taifa, Bodi ya Tumbaku, ujenzi na
fedha.
Naye
Mkuu wa Takukuru mkoani Shinyanga, Gasto Mkono alisema katika kipindi
cha miezi mitatu wamepokea taarifa 39 kutoka kada mbalimbali ikiwemo
kufuatilia miradi ya maendeleo iliyojengwa chini ya kiwango.
Alisema
tayari kesi 13 zipo mahakamani zikiwemo kesi zingine mpya nne
zilizofunguliwa kipindi hicho zinazohusika na masuala ya utoaji hongo
huku miradi saba ikiwa katika uchunguzi na miwili imebainika kuwa na
kasoro.
Mkono
aliyekuwa anazungumza na waandishi wa habari alisema kutokana na
kukithiri kwa rushwa ndogondogo katika kada mbalimbali kumesababisha
wananchi kuichukia Serikali.
“Machi
21, mwaka huu, Alex Filipo ambaye ni askari wilayani Kishapu
alituhumiwa kuomba kiasi cha Sh milioni moja kutoka kwa mganga wa
kienyeji, Jidala Ngusa aliyemkamata kwa kufanya uganga bila kibali
askari alikamatwa akipokea kiasi cha Sh 50,000 ikiwa sehemu ya
mwendelezo wa malipo ya fedha hizo,” alisema Mkono.
Alisema
Takukuru inaendelea kutoa elimu katika jamii na idara zinazolalamikiwa
kwa vitendo vya rushwa mkoani hapa ni serikali za mitaa, ardhi, afya,
sekta binafsi, polisi, magereza, mahakama, elimu na kwenye vyama vya
siasa hasa nyakati za uchaguzi.
Post a Comment