Ofisi ya Elimu wilayani Kisarawe, Mkoa wa Pwani imelazimika kuwapa likizo
walimu saba wa Shule ya Msingi Mingwata ili kuwajenga kisaikolojia baada
ya kukithiri kwa matukio ya kishirikina yanayowakumba katika shule
hiyo.
Walimu hao wanakumbana na matukio ya ajabu ikiwamo
kujikuta uchi, kupigwa fimbo na mtu asiyeonekana na kulazwa nje ya
nyumba zao.
Mmoja wa walimu walioathirika na matukio hayo,
Emmanuel Shaaban alisema yeye na familia yake hawana raha kutokana na
matukio hayo kwa kuwa usiku huvuliwa nguo na kujikuta wamelazwa sehemu
nyingine, huku wakiwa wamechanjwa kwa wembe mwili mzima.
“Tarehe
26 mwezi wa pili, siku ya Alhamisi sitaisahau kabisa. Ndiyo siku ambayo
nilikatwa viwembe mwili mzima na hali yangu ilikuwa mbaya, niliishiwa
nguvu na mwili ukawa na ganzi na nilipokwenda hospitali niliambiwa sina
ugonjwa,” alisema Shaaban.
Alisema alipotoka hospitali alikwenda
kijijini kwao mkoani Mwanza na huko aliendelea kuwa na hali mbaya
kutokana na kuzimia mara kwa mara kwa sababu ya maumivu ya kichwa hadi
alipotibiwa kienyeji.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Mikidadi
Mbelwa alisema awali alikuwa akiona vituko usiku na mchana, lakini
alivumilia huku akitunza siri bila kuwaeleza wenzake ili asiwakatishe
tamaa.
Mbelwa alisema baadhi ya matukio aliyokutana nayo ni
kuvuliwa nguo usiku, kulazwa eneo jingine, kuchapwa viboko, kumwagiwa
damu kwenye korido ya nyumba, kuchanjwa kwa wembe, kuzungukwa na nyoka
mwilini, kuona mtu na kisha anapotea na kutupwa kwenye mashimo.
Mzazi
wa watoto wanaosoma katika shule hiyo, Asha Kondo alikiri kuwapo kwa
matukio ya watoto kuugua na kuanguka hadi uongozi wa kijiji ulipopeleka
mganga wa kienyeji kutoa kinachodaiwa ni uchawi.
Mratibu wa Elimu wa Kata ya Marui, Damaru Charles alisema amekuwa akipokea malalamiko hayo na kuyawasilisha ngazi za juu.
Ofisa
Elimu Msingi wilayani hapa, Aurelia Rwenza alisema tatizo hilo linawapa
shida walimu na kurudisha nyuma maendeleo ya elimu katika sehemu hiyo.
“Kwa kweli walimu wameathirika, hivi sasa tunatakiwa kuwajenga kisaikolojia,” alisema.
Post a Comment